Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICAO imekuwa mshirika tupatapo majanga:Ban

Miaka 70 ya mkataba wa kimataifa wa usalama wa anga ulioanzisha ICAO

ICAO imekuwa mshirika tupatapo majanga:Ban

Shirika la kimataifa la usalama wa anga, ICAO limekuwa mstari wa mbele kusaidia Umoja wa Mataifa kushughulimia masuala muhimu duniani, amesema Katibu Mkuu Ban Ki-Moon wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya kuanzishwa kwa mkataba wa kimataifa wa usalama wa anga.

Shughuli hiyo imefanyika Chicago, Marekani makao makuu ya ICAO ambapo Ban ametaja masuala muhimu ambayo shirika hilo limetoa usaidizi kuwa ni pamoja na afya, usalama na mazingira.

Ametola mfano afya akisema ugonjwa wa Ebola ulipoibuka, ICAO ilijibu hofu za watu kwa kutoa maelezo sahihi.

(Sauti ya Ban)

“ICAO ilisimama kidete na Shirika la afya duniani, WHO dhidi ya vizuizi vya safari na biashara ambavyo vilizuia jitihada zetu za kupeleka matabibu na vifaa tiba. ICAO ilipigia debe mikakati ya kuhakikisha visa vinavyodhaniwa kuwa ni Ebola vinashughulikiwa kwa usalama bila kueneza zaidi ugonjwa huo.”

Kuhusu usalama amesema ndege ya abiria ilipoanguka Ukraine mwezi Julai, na Umoja wa Mataifa kutaka uchunguzi, ICAO ilisaidia kutoa taarifa za awali na uchunguzi unaendelea.  

Halikadhalika mazingira..

“Kupitia ICAO, serikali na sekta ya usafiri wa anga wameahidi kuboresha kwa asilimia mbili kwa mwaka kiwango cha mafuta ya ndege kisichoharibu mazingira ifikapo mwaka 2020. Halikadhalika wanasaidia kuendeleza teknolojia mpya kwenye sekta hiyo zisizoharibu mazingira.”