Bado watu Milioni 19 hawafahamu iwapo wana kirusi cha Ukimwi:Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana bado kuna changamoto ikiwemo kufikishia huduma watu Milioni 19 wasiofahamu iwapo wana kirusi cha Ukimwi. Amesema idadi hiyo ni kati ya watu Milioni 35 wanaoishi na virusi vya Ukimwi na hivyo kutishia kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana wakati huu ambapo harakati za kudhibiti Ukimwi zinakumbwa na changamoto ya Ebola.
Makundi muhimu mathalani watoto wawili kati ya watatu wanaohitaji huduma dhidi ya Ukimwi hawaipati halikadhalika wasichana barubaru akitolea mfano maeneo ya Ulaya MAshariki, Asia ya Kati na MAshariki ya Kati.
Ban amesema mifumo ya afya pekee haitoshelezi kutoa huduma bora, bali pia haki ya kijamii, matumizi bora ya sayansi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha kwa uwiano sahihi bila kusahamu mfumo wa afya unaojali watu.
Kwa mantiki hiyo ametaka viongozi duniani kukumbuka ahadi yao ya kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030 akisema mpango wa kuongeza kasi uliozinduliwa wiki iliyopita unaweza kufanikisha lengo hilo.