Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takwimu zimewezesha kuonyesha mwelekeo wa majaliwa ya watoto: UNICEF

Takwimu zimewezesha kuonyesha mwelekeo wa majaliwa ya watoto: UNICEF

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya watoto duniani imesema utaratibu wa kutoa takwmu za watoto ulioanza miaka 30 iliyopita umewezesha kuonyesha hali halisi ya mwelekeo wa kundi hilo na hivyo kuweka mazingira ya kuhakikisha haki zao za msingi zinazingatiwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF lililoandaa ripoti hiyo limesema maisha ya mamilioni ya watoto duniani kote yameokolewa kutokana na takwimu mbali mbali ikiwemo majisafi, utapiamlo na elimu.

Mathalani UNICEF imesema kuboreshwa kwa huduma za majisafi na kujisafi kumeokoa maisha ya watoto Milioni 90 ambao wangalifariki dunia kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano iwapo wasingalipatiwa huduma hizo.

Mmoja wa wataalamu wa UNICEF Tessa Wardlaw amesema ripoti imeweka bayan tofauti katika kusongesha haki kuu nne za mtoto ikiwemo Kuishi, Kuendelezwa, Kushirikishwa na Kulindwa.

Bi. Wardlaw amesema maendeleo zaidi yanaweza kupatikana iwapo dunia itafahamu ni watoto gani wanapuuzwa zaidi, wapi watoto wa kike na wa kiume hawaendi shule, wapi magonjwa yameena zaidi na wapi huduma za msingi za kujisafi hazipatikani.

Ripoti hiyo inatanabaisha kuwa takwimu pekee hazibadilishi dunia bali zinawezesha mabadiliko duniani kwani watunga sera huzitumia kufanya uamuzi na hata jamii na watoto wanaweza kuzitumia ili kuwajibisha mamlaka husika.