Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jengo la Empire State New York kun’goa nanga ya kampeni dhidi ya ukatili kwa wanawake

Jengo la Empire State jijini New York. (Picha hisani ya ESRT Empire State Building, L.L.C.)

Jengo la Empire State New York kun’goa nanga ya kampeni dhidi ya ukatili kwa wanawake

Taa katika jengo mashuhuri jijini New York, Empire State, kuanzia machweo ya leo jumatatu zitawaka rangi ya chungwa kuashiria siku ya kimataifa ya kupiga vita aina zote za ukatili dhidi ya wanawake.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ataungana na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja huo linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women Phumzile Mlambo-Ngucka pamoja na mwigizaji mashuhuri Teri Hatcher kuwasha taa hizo wakati wa jioni.

Rangi ya chungwa imechaguliwa na Umoja wa Mataifa kuwa rangi ya kimataifa kuchagiza watu duniani kote kuchukua hatua za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.

Hatua hiyo ya leo pia inang’oa nanga siku 16 za harakati dhidi ya ukatili wa kijinsia ambapo jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa nalo litakuwa na rangi hiyo ya chungwa wakati huo huo wa jioni.

Imekuwa ni utamaduni kwa nyakati mbali mbali za mwaka jengo la Empire State jijini New York kubadili rangi ya taa zake kama ishara ya kutambua matukio au shughuli za mashirika mbali mbali.