Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaunga mkono miongozo inayolenga kusaidia wanawake wasaka hifadhi

Mwanamke mkimbizi kutoka Syria akiwa katika moja ya kambi za wakimbizi huko Bekaa nchini Lebanon. (Picha:UNHCR/ A. McConnell)

UNHCR yaunga mkono miongozo inayolenga kusaidia wanawake wasaka hifadhi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limekaribisha miongozo mipya ya kimataifa inayotaka nchi kuwa na mitazamo ya kijinsia zinaposhughulikia mahitaji ya wakimbizi wasio na utaifa.

Miongozo hiyo imetolewa leo na kamati ya Umoja wa Mataifa ya kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake ambapo inataka masuala ya wanawake walio ukimbizini, wasaka hifadhi au wasio na utaifa yanaposhughulikiwa yazingatie ukatili wanaokumbana nao mara kwa mara.

Mkurugenzi wa UNHCR anayehusika na hifadhi za kimataifa Volker Türk amesema wanachoshuhudia sasa ni matukio mengi ya wanawake kukimbia nchi zao na kusaka hifadhi ugenini kutokana na ukatili wa kijinsia wanaokumbana nao.

Kwa mantiki hiyo amesema pendekezo hilo jipya linapaswa kusaidia nchi katika kushughulikia visa vya aina hiyo kwa njia sahihi zaidi.

Kamati imesema kushindwa kuwa na mtazamo wa kijinsia, mara nyingi husababisha kupitishwa kwa uamuzi wa hifadhi unaowanyima wanawake na wasichana wengi hifadhi ya kimataifa.