Ban asema Tunisia ni mfano wa matunda ya vuguvugu lenye kuleta utulivu

10 Oktoba 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema Tunisia ni mfano wa matunda bora yanayotokea pindi serikali inaposikiliza mahitaji ya wananchi wake na kuyafanyia kazi.

Ban amesema hayo mjini Tunis kwenye mkutano na waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na Rais Mohamed Marzouki.

Amesema vuguvugu la nchi za kiarabu lilipoanza, Tunisia ilisimamia misingi yake na kutokana na maadili, uongozi bora na ushirikishaji wa raia, mabadiliko yalifanyika kwa amani na kuleta utulivu.

Amesifu mafanikio yaliyopatikana Tunisia akisema Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa mshirika wakati nchi hiyo inaendelea kujijenga.

Ban amesema yeye na Rais Marzouki wamejadili pia hali ya Libya ambapo wameonyesha wasiwasi, lakini amemshukuru kwa vile wanavyounga mkono harakati za Umoja wa Mataifa za kufanikisha mchakato wa kisiasa.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter