Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twahitaji wadau zaidi kuimarisha mipango yetu ya ulinzi: Ladsous

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous. (Picha:UN/Eskinder Debebe)

Twahitaji wadau zaidi kuimarisha mipango yetu ya ulinzi: Ladsous

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, Hervé Ladsous amesema ni jambo la kusikitisha kuwa walinda amani Tisa wamekuwa wahanga wa kitendo chao cha kujitolea kulinda amani ya raia nchini Mali.

Ladsous amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Bamako, ikiwa ni siku nne tangu kuuawa kwa walinda amani hao Tisa kutokaNigerwakati wakiwa kazini kaskazini mwa Mali.

“Nataka kuwaambia hawa majihadi na vikundi vingine vyenye msimamo mkali kwamba vitendo vyao vya kigaidi havipaswi kupita bila kuadhibiwa. Kitendo hiki ni cha kiwango kikubwa na ni lazima tuidhibiti na tuwe na mpango madhubuti. Nadhani ni dhahiri tunahitaji wawezeshaji zaidi kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ambayo sisi tunaweza kufanya kazi katika usalama ndani ya vitisho hivi."

Walinda amani hao wanatekeleza majukumu yao chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini, MINUSMA ambapo tangu kuanzishwa kwake mwaka jana walinda amani wapatao 30 wameuawa wakiwa kazini.

Wakati huo huo msemaji wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa Bwana Ladous kesho atahutubia Baraza la usalama kwa njia ya video kutoka Bamako kuhusu hali ya usalama nchini Mali.

===