Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mmea wa Teff unafaa kwa wagonjwa kisukari aina ya II: FAO

Mmea wa Teff. Picha: FAO

Mmea wa Teff unafaa kwa wagonjwa kisukari aina ya II: FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limetangaza mmea wa Teff kuwa ni zao la kiasili kwa mwezi huu wa Oktoba ikiwa ni mpango wake wa kutaja mazao hayo yaliyosahaulika lakini yana umuhimu kwa maisha ya binadamu. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Nafaka hiyo hupatikana Ethiopia na Eritrea ambako ndiyo asili yake na huwa na rangi nyeupe, nyekundu au mchanganyiko ikichangia theluthi mbili ya virutubisho vya protini kwenye mlo wa wakazi wa nchi hizo.

Kwa sasa zao hilo linalimwa pia kama zao la nafaka maeneo ya kaskazini mwa Kenya, FAO ikisema linaweza tumika kutengeza kinywaji au mlo ambapo mara baada ya kuvunwa hulowekwa angalau kwa siku tatu na hatimaye kusagishwa kuwa unga unaotumika kutengeneza uji na pia chapatti maji ziitwazo Enjera.

FAO pamoja na kueleza mapishi yake, imeweka bayana kuwa Teff inafaa kwa wagonjwa wenye kisukari aina ya II na pia zao lina manufaa kwa wakulima wadogo kwa kuwa linastahimili mtwamo wa maji na linaweza kuhifadhiwa kwa muda bila kushambuliwa na wadudu.