Usambazaji misaada Syria bado unazuiwa na wapiganaji- Mkuu wa OCHA

30 Septemba 2014

Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura, Valerie Amos, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa makundi yanayopigana nchini Syria bado yanaendelea kuyazuia mashirika ya kibinadamu kufikisha misaada kwa walengwa, licha ya Baraza hilo kupitisha maazimio yaliyozitaka pande zinazozozana kuruhusu na kuwezesha misaada hiyo kusambazwa. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Bi Amos ameyasema hayo wakati Baraza la Usalama likikutana kujadili hali Mashariki ya Kati, ambapo amewasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu utekelezaji wa azimio namba 2139 lililopitishwa miezi saba iliyopita, na azimio namba 2165 lililoptishwa miezi miwili iliyopita, yote yakihusu hali ya kibinadamu nchini Syria

“Maazimio hayo yanalenga kukomesha kuenea kwa machafuko na ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na ile ya kibinadamu dhidi ya watu wa Syria. Yanalenga pia kuboresha ufikiaji wa wale wenye mahitaji. Lakini machafuko yanaendelea bila utulivu wowote kote nchini Syria, hata katika maeneo ambayo awali hayakuathiriwa, na watu wanalaazimika kila siku kuhama na kuwa katika ukiwa.”

Bi Amos amesema kuwepo kwa makundi yenye silaha na mapigano, kunafanya ufikishaji misaada kwa walengwa kuwa mgumu na hatari, huku uhaba wa ufadhili ukilazimu mashirika ya misaada kusitisha shughuli za kibinadamu

“Bila ufadhili zaidi, Shirika la Mpango wa Chakula litalazimika kukomesha operesheni zake kabisa miezi miwili ijayo. Migawo tayari imepunguzwa ili kuweza kuwafikia watu wengi iwezekanavyo. Msimu wa baridi unakaribia, na vifaa muhimu vinahitajika kuwalinda watu kutokana na baridi.”

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter