Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazingira kwenye kituo cha wakimbizi Bentiu si mazuri: UNMISS

Wakimbizi wa ndani wanaoishi katika maeneo yanayolindwa yaliyokumbwa na mafuriko. Picha: UNMISS / JC Mcilwaine

Mazingira kwenye kituo cha wakimbizi Bentiu si mazuri: UNMISS

Mkuu wa masuala ya usaidizi wa kibinadamu Sudan Kusini, Toby Lanzer ametembelea eneo linalohifadhi wakimbizi wa ndani huko Bentiu jimbo la Unity na kusema kuwa hali si nzuri kwani kituo hicho walichohifadhiwa kimefurika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Taarifa zaidi na Abdullahi Boru.

(Taarifa ya Abdullahi)

Akiwa ameambatana na mabalozi wa Uingereza na Uholanzi kujionea hali halisi Lanzer amesema hali ni mbaya kwa wakimbizi hao 40,000 waliosaka hifadhi kwenye kituo hicho cha UNMISS lakini hawana la kufanya kutokana na tishio la usalama huko makwao.

Lanzer ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS amesema kituo kiko bondeni, na mfululizo wa mvua zinazoendelea kunyesha unafanya maji yajae na kufikia usawa wa kiuno na hivyo maisha ya watu kuwa hatarini.

(Sauti ya Lanzer)

“Hawana pahala pakavu pa kuishi, hawana kuni kwa ajili ya kupikia, hali ya kujisafi imezorota sana. Kwa sasa choo kimoja kinatumiwa na watu zaidi ya 100 kwa vile vinavyofanya kazi, na mashiriki ya misaada yanashirikiana na UNMISS angalau kufanya hali hii mbaya sana iwe nzuri kidogo.”

Lanzer amesema ingawa maeneo ya mijini kama vile Bentiu kati ni makavu, watu wanachagua kuishi kwenye kituo hicho kilichofurika maji kutokana na hofu ya usalama.

Amerejea wito wa Umoja wa Mataifa wa kutaka amani ya kudumu ili wananchi waweze kurejea kwenye maeneo yao na kuendelea na shughuli za kujipatia kipato.