Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali nchini Libya ni ya kutia hofu, asema Mitri

UN Photo/Devra Berkowitz
Tarek Mitri, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya.

Hali nchini Libya ni ya kutia hofu, asema Mitri

Baraza la Usalama leo limekutana kujadili kuhusu Lybia na kazi za Ujumbe wa Umoja wa Matiafa nchini humo, UNSMIL. Tarek Mitri, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa UNSMIL, amewaambia wanachama wa baraza hilo kwamba raia wa Lybia wanazidi kutiwa hofu kadri mzozo unavyoendelea kuongezeka Lybia.

“ Kasi ya mabadiliko ya hali ya usalama mjini Tripoli kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita ni dalili ya tatizo kubwa la kisiasa linaloathiri nchi na kuhatarisha utaratibu mzima wa kisiasa”

Ameeleza kwamba mapigano baina ya waasi katika maeneo ya uwanja wa ndege wa Tripoli mwanzo mwa Julai yamesababisha zaidi ya vifo 30 pamoja na kusitisha safari zote za ndege.

Halikhadalika, ameliambia Baraza la Usalama kwamba UNSMIL imeshindwa kuongoza mazungumzo baina ya pande zote wakati wa maandalizi ya uchaguzi uliofanyika tarehe 25, Juni. Uchaguzi huo, amesema, umetekelezwa kwenye hali ya ghasia, mgombea mmoja na mwanaharakati mmoja wa haki za binadamu, Salwa Bugaighis, wakiuawa.

Amesema, UNSMIL imeshindwa kuhakikisha usalama wa wafanya kazi wake:

“ Kutokana na kwamba hali inazidi kuzorota, uwanja wa ndege umefungwa, usalama wa UNSMIL na wafanyakazi umo hatarini, wakishindwa kuendelea na shughuli zao. Maamuzi yamechukuliwa kupunguza na hatimaye kuwaondoa kabisa wafanyakazi wa kimataifa waliomo Lybia. Hayo yalikuwa maamuzi magumu”