Ban Ki Moon akutana na rais wa Haiti na Jamhuri ya Dominika

16 Julai 2014

Akihitimisha ziara yake nchini Haiti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amekutana na rais wa nchi hiyo, Bwana Logan Martelly akiwapongeza raia wa Haiti kwa bidii yao katika kujenga upya nchi baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililoathiri nchi yao mwaka 2010, na licha ya hali mbaya ya kiuchumi.

Amesifu serikali ya Haiti kwa kujitahidi kupunguza visa vya kipindupindu, akisema kwamba Umoja wa Mataifa, kwa kupitia mradi mpya wa usafi aliouzindua wakati wa ziara yake, utaendelea kuimarisha miundombinu ya maji safi ili kupambana na ugonjwa huo, akisema:

“ Nadhani raia wa Haiti wamepitia mateso ya kutosha. Wanastahili kuwa na mustakhabali wa matumaini, uakilishi kamili wa kisiasa, umoja wa kijamii, maendeleo ya kiuchumi na uendelevu wa mazingira. Ndiyo maana nipo hapa, na ni mara ya tano naja hapa.”

Baada ya hapo, amewasili nchini Jamhuri ya Dominika ambapo amekutana na rais Danilo Medina, akisema nchi hiyo inastahili kusifiwa kwa kuwekeza asilimia 4 ya kipato cha nchi katika sekta ya elimu, akimpongeza rais kuwa na ndoto ya muda mrefu kwa nchi yake, na kujitahidi kuongeza usalama wa chakula na kupambana na janga la ukimwi.

Halikadhalika, amesisitiza umuhimu wa Jamhuri ya Dominika kutahadhari na matokeo ya mabadiliko ya tabianchi, akisema kwamba nchi hiyo inaweza kuathirika na madhara mbalimbali yatokanayo na hali ya hewa.

Hatimaye, ameomba mamlaka za Jamhuri ya Dominika kuendelea kuchukua hatua ili kuwapatia uraia watu wenye asili ya Haiti waliozaliwa nchini humo .

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter