Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 10 Yemen waathirika na njaa

Yemen. Picha@OCHA/Eman Al-Awami(UN News Centre)

Watu milioni 10 Yemen waathirika na njaa

Utafiti uliofanyika nchini Yemen na Shirika la Mpango wa chakula Duniani WFP na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Watoto UNICEF, unaonyesha kwamba bado watu milioni 10, yaani asilimia 40 ya watu waliopo Yemen, wanakumbwa na ukosefu wa usalama wa chakula.  Taarifa Zaidi na Priscilla Lecomte

Kwa mujibu wa WFP, katika watu hawa, ni milioni tano ambao wako kwenye hali mbaya zaidi ya kuathirika na njaa na kuhitaji msaada wa chakula. Halikadhalika, kiwango cha utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni juu ya kiwango cha dharura kilichobainiwa na watalaam wa kimataifa.

Msemaji wa WFP, Elisabeth Byrs, amesema sababu za mzozo huo ni mbili:

“ Kuna sababu za hali ya hewa, na pia hali ya usalama. Sasa ukosefu wa usalama wa chakula unaweza kuathiri utulivu wa nchi kisiasa. Ili utaratibu wa kisiasa ufanikiwe, watu wanahitaji kuwa na maisha ya kawaida bila kuwa na wasiwasi wa chakula chao cha kila siku. Ni msingi wa lazima kwa utulivu wa kisiasa kwa baadaye”

Ameeleza pia kwamba tofauti ni kubwa katika mashariki mwa nchi na majimbo ya kaskazini na magharibi ambapo hali ni mbaya zaidi, hasa kwa watoto ambao wamechelewa kukua kimwili na kiakili, akiongeza kwamba watoto hawa watabaki wadhaifu kwa maisha yao yote.

Byrs amesema, WFP na UNICEF wataendelea kusambaza msaada kwa kulenga majimbo yaliyoathirika zaidi.