Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yasaidia wakimbizi wa Nigeria nchini Cameroon

Wakimbizi wanaokimbia ukatili wa Boko Haram katika taifa la Borno, Nigeria. Picha: IRIN/Anna Jefferys(UN News Centre)

WFP yasaidia wakimbizi wa Nigeria nchini Cameroon

Kufuatia machafuko yanayoendela kaskazini mwa Nigeria, raia wengi wamekimbia na kutafuta hifadhi katika nchi jirani ya Cameroon ambapo Shirika la Mpango wa Chakula duniani WFP linawapa usaidizi, licha ya mazingira yasiyo salama na matatizo ya usafiri.

Elizabeth Brys ambaye ni Msemaji wa WFP ameeleza kwamba hii ni mara ya kwanza kwa WFP kutoa usaidizi karibu na mpaka wa Nigeria akisema;

“ Watu hawa wanakimbia vijiji ambavyo viliteketezwa moto, ili waokoe maisha yao. Kwa ujumla ni watu 8,000 waliokimbia Nigeria tangu mwezi wa Mei, na kutafuta hifadhi katika maeneo hayo ya kaskazini mwa Cameroun.”

Bi Byrs amesema jamii za Cameroon zimekuwa zikiwasaidia wakimbizi hao lakini akiba za vyakula zimeaanza kupungua na wengi wa wakimbizi wanaowasili upya hawana lishe ya kutosha.

“Wasiwasi wetu hasa ni kuhusu viwango vya utapiamlo tulivyoshuhudia katika watoto. Tathmini iliyofanyika mwisho mwa mwezi wa Juni ilionyesha viwango vya juu katika watoto waliofika hivi karibuni. Kiwango cha utapiamlo katika wilaya ya Waza kilifika asilimia 25 juu zaidi ya kiwango cha dharura ambacho ni asilimia 15”.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, zaidi ya watu 600,000 wamekimbia makwao kwenye maeneo ya kaskazini mwa Nigeria ambako mashambulizi ya makundi yaliyojihami yanatokea mara kwa mara.