Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen kuna tatizo kubwa duniani lililofichwa: UM

Yemen. Picha@OCHA/Eman Al-Awami(UN News Centre)

Yemen kuna tatizo kubwa duniani lililofichwa: UM

Nchi ya Yemen imo katika hali mbaya ya kibinadamu, inayozidi hali za matatizo mengi duniani, wamesema leo wataalam wawili wa Umoja wa Mataifa wakizungumza na waandishi wa habari.

Wamesema nchi hiyo imedhoofika sana, na mwelekeo si mzuri kutokana na viashiria mbalimbali. Mkuu wa operesheni wa ofisi ya usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa, OCHA,

John Ging, aliyehitimisha ziara yake nchini humo, amesema, watu zaidi ya milioni 10 wamekumbwa na ukosefu wa usalama wa chakula, lakini ni watu milioni moja tu ndio wamepata msaada wa kibinadamu.

Mizizi ya matatizo yanayoendelea nchini humo ni ya kisiasa na kiuchumi, ameongeza John Ging, akisema pia uchumi wa nchi hiyo unakaribia kufilisika. Shida nyingine ni utumiaji wa mairungi, ambao ni janga kubwa kwa nchi hiyo, kwa mujibu wa mtalaam huyo akisema asilimia 70 ya matumizi ya maji ni kwa ajili ya kilimo cha mairungi.

Amesisitiza kuwa ingawa usaidizi wa kibinadamu wa dharura si suluhu kwa Yemen, wakati suluhu ya kudumu ikihitajika, bado utoaji wa usaidizi huo ni lazima hivi sasa ili kuokoa maisha ya wananchi.

Kwa mujibu wa Ted Chaiban, Mkurugenzi wa mipango ya Dharura katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, ambaye alikuwa naye ziarani Yemen, utapiamlo ndiyo shida ya kwanza nchini humo:

“ Ukiangalia hali ya utapiamlo, mtoto mmoja kati ya watano ameathirika na utapiamlo, na asilimia 58 wakiwa wamedumaa. Ina maana kwamba, baada ya Afghanistan na kabla ya nchi zingine zote za dunia, Yeman iko na kiwango kikubwa cha utapiamlo. Ni kitu ambacho watu hawajui wakifikiria Yemen. Inashangaza sana. Hali hiyo imeendelea kwa miaka, ni matokeo ya umaskini, kutoendelea kwa uchumi, na pia mzozo wa kisiasa unaoendelea tangu miaka mitatu iliyopita".

Changomoto nyingine kwa watoto ni uandikishaji wa watoto shuleni na ndoa za utotoni. Lakini jitahada za mashirika ya kimataifa zinaendelea, amesema Chaiban, UNICEF ikiwa imefanikiwa kutoa chanjo za polio kwa asilimia 98 ya watoto nchini humo.