Ban ataka viongozi wa dunia wachukue hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

11 Aprili 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameshiriki mkutano wa viongozi kuhusu mabadiliko ya tabianchi huko Washington D.C na kurejelea wito wake wa umuhimu wa kupunguza viwango vya joto chafuzi.

Amesema suala hilo linapaswa kuwa ajenda muhimu kwa viongozi wanapoangazia suala la maendeleo endelevu kwa hivyo ni vyema kufikia makubaliano ya dunia kuhusu mabadilko ya tabia nchi kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mabadiliko ya tabianchi ni jambo linaloainisha nyakati za sasa. Yamekuwa na madhara maeneo yote duniani na kutishia usalama na maendeleo amesema Katibu Mkuu kwenye mkutano huo uliohudhuriwa pia na Rais wa Benki ya dunia Jim Yong Kim.

Bwana Ban alizungumza pia katika mkutano kuhusu usafi na maji kwa wote ambapo alisema bado rasilimali hiyo bado ni adimu kwa wakazi wengi duniani akitolea mfano barani Afrika akisema huduma ya maji ni duni na inasababisha zaidi umaskini.

“Iwapo tunafikia maelngo yetu,tutaondoa ukosefu wa usawa kati ya matajiri na maskini, miji na maeneo ya pembezoni na wanaume na wanawake ambao afya zao mara nyingi ziko hatarini kutokana na huduma zisizo bora za kujisafi.”

Bwana Ban amesema siri ya mafanikio ni kuwa na uwekezaji sahihi, kujizatiti kutekeleza na kusimamia vyema na hatimaye kuhamasisha mijadala kuhusu umuhimu wa majisafi hususan kwenye maeneo ambako hoja nyingine mathalani huduma za vyoo haziwezi kujadiliwa.