UNHCR yaokoa 13 waliokuwa warejeshwe Somalia

9 Aprili 2014

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR nchini Kenya limesema limeweza kuwaokoa raia 13 wa Somalia waliokuwa warejeshwe makwao leo asubuhi.

Naibu Mwakilishi mkazi wa UNHCR nchini humo Abel Mbilinyi ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa katika mahojiano maalum kuwa watu hao walikuwa miongoni mwa waliokamatwa mwishoni mwa wiki kutoka eneo la Eastleigh mjini Nairobi na waliweza kuwaokoa baada ya kupata habari kuwa wanasafirishwa.

(Sauti ya Abel)

Amesema watu hao sasa wamerejeshwa kituo cha polisi na kesho Alhamisi UNHCR itafuatilia kuona iwapo wameachiliwa kutoka mikono ya polisi.

Halikadhalika Bwana Mbilinyi amesema pamoja na kutambua umuhimu wa ulinzi na usalama Kenya ni lazima sheria za kimataifa zizingatiwe akiongeza kuwa UNHCR na serikali ya Kenya wamefikia makubaliano.

(Sauti ya Abel)

Kwa mujibu wa UNHCR asubuhi ya Jumatano ndege iliyokuwa na watu takribani 80 iliondoka Nairobi kuelekea Mogadishu ikirejesha nyumbani watu hao na kwamba shirika hilo halikupata fursa ya kuzungumza nao kabla ya kuondoka.