Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aitaka CAR ijizuie kutumbukia kwenye mauaji ya kimbari

Ban aitaka CAR ijizuie kutumbukia kwenye mauaji ya kimbari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Kin Moon amewataka wananchi, viongozi wa dini pamoja na pande kinzani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kujizuia ili kuilinda nchi yao dhidi ya kile alichokiita harufu ya mauaji ya kimbari.

Ban ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na baraza la mpito la CAR mjini Bangui ambapo amesema mgogoro wa kidini ni dhahiri akitolea mfano kuwa waislamu wamekimbia huku wakristo wakiwa katika hatari ya kifo kutokana na imani na msimamo wao.

Katibu Mkuu ambaye anatarajiwa kuwaRwandakwa ajili ya maadhimisho ya miaka 20 ya mauaji ya kimbari nchini humo April 7, amelitaka taifa hilo kutotumbukia katika kumbukumbu kama hiyo ambayo amesema sio nzuri na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuendelea kuisaidia CAR ili kunusuru machafuko zaidi.

Ametambua juhudi za Umoja wa Ulaya kwa uamuzi wake wa kupeleka vikosi zaidi siku za usoni na kupongeza muungano wa Afrika na majeshi ya Ufaransa (MISCA) kwa kazi ya kulinda amani lakini akaongeza kuwa ametaka kuongezwa kwa vikosi na askari walinda amani na kulitaka baraza ala usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha vikosi vya MISCA kuwa operesheni za ulinzi wa amani za UM.

Ban amehitimisha ujumbe wake kwa kuwataka watu wa CAR kuamua mustakabali mwema kwa ajili ya nchi yao akisema uchaguzi wa kujenga au kubomoa mustakabali wao na watoto wao uko katika mikono yao.