Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Ukraine umegeuka kuwa mzozano kuhusu Ukraine: Ban

Mzozo wa Ukraine umegeuka kuwa mzozano kuhusu Ukraine: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, amesema kuwa kilichoanza kama mzozo wa Ukraine, sasa kimebadilika kuwa mzozano kuhusu Ukraine. Bwana Ban amesema hayo wakati akiwahutubia waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini, New York, baada ya kulihutubia Baraza la Usalama kufuatia ziara yake iliyompeleka Urusi, Ukraine, Uholanzi alikohudhuria mkutano wa kuzuia ugaidi wa nyuklia, na hatimaye huko Greenland, alikokwenda kufanya tathmini ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kuhusu mzozo wa Ukraine, Bwana Ban amesema tangu mwanzoni, lengo lake limekuwa ni kutafuta suluhu la amani na la kidiplomasia kwa mzozo huo, kwa misingi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa.

“Ninatoa wito kwa viongozi wa Urusi na Ukraine kutuliza hali, kuepukana na vitendo vya kiholela na kuanza mara moja mazungumzo ya moja kwa moja yanayoweza kujenga, ili kutatua matatizo yote. Wakati huu wa hali tete, hata cheche ndogo zinaweza kulipua moto mkubwa wa madhara ambayo hayakutarajiwa. Ninasikitika pia sana kuwa migawanyo katika jamii ya kimataifa kuhusu suala hilo, inaweza kuongeza kuzuia uwezo wetu kushughulikia masuala mengine muhimu: mizozo na masuala ya kibinadamu ya dharura.”

Bwana Ban amesema ametoa wito kwa wito kwa Baraza la Usalama lilishghulikie suala la Ukraine haraka

“Kuna masuala mengi ya kipindi kirefu, kama vile malengo ya maendeleo ya milenia, maendeleo endelevu na mabadiliko ya tabianchi. Nasikitika kuwa masuala haya yote muhimu hayajapewa kipaumbele na viongozi wa kimataifa kwa sababu ya mizozo hii yote kikanda, kama Ukraine, Syria na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Sasa ndio wakati wa mazungumzo na amani.”

Bwana Ban pia amezungumza kuhusu mkutano alioshiriki kuhusu kuzuia ugaidi wa nyuklia

“Niliungana na viongozi wengine wa kimataifa katika kumulika haja ya kuchukua tahadhari dhidi ya hatari ya ugaidi wa nyuklia. Ushirikiano wa kimataifa utakuwa muhimu, siyo tu katika kuzuia usambazaji wa vifaa vya nyuklia, lakini pia katika kuendeleza uondoaji wa silaha za nyuklia, ambalo ni hakikisho bora dhidi ya tishio hili.”

Kuhusu ziara yake nchini Greenland, na suala la mabadiliko ya tabianch, Bwana Ban amesema

“Niliweza kujionea mwenyewe athari za suala la mabadiliko ya tabianchi. Barafu inayeyuka kwa kasi sana. Ingawa naona fahari kuhusu busara ya maisha ya watu wa Greenland ambao wamekuwa wakiishi kwa kujali mazingira, tegemeo lao la maisha limo hatarini kwa sababu ya kuyeyuka kwa barafu. Natumai viongozi wa kimataifa watakuja na utashi thabiti wa kisiasa kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi Septemba 23.”