Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Athari za uhaba wa maji na uhakika wa chakula kuangaziwa kwenye mkutano wa NENA.

Athari za uhaba wa maji na uhakika wa chakula kuangaziwa kwenye mkutano wa NENA.

Uhaba wa maji na uhakika wa chakula ni ajenda kuu ya mkutano wa 32 wa nchi za Afrika Kaskazini na baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati, NENA utakaoanza jumatatu ijayo huko Roma, Italia, limesema shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kama anavyoripoti Assumpta Massoi.

(Ripoti ya Assumpta)

Wakati upatikanaji wa maji kwenye nchi za NENA ukikadiriwa kupungua kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2050, FAO inasema kuwa mahitaji ya maji kwa kila mtu kwenye eneo hilo yameongezeka kwa theluthi mbili katika miaka 40 iliyopita.

FAO imesema hali hiyo imeibua hofu kuhusu ongezeko la mahitaji wakati huu ambapo mabadiliko ya tabianchi yanakuwa changamoto kubwa kwa upatikanaji kwa rasilimali hiyo na hivyo kuathiri hata shughuli za kilimo.

Hivyo mawaziri kutoka nchi hizo watakutana ili kuweka mkakati wa kupatia suluhu jambo hilo. Pasquale Steduto ni Mwakilishi wa FAO kanda ya Afrika Kaskazini na Mashariki.

(Sauti ya Pasquale)

Zaidi ya asilimia 60 ya maji yatumikayo kwenye nchi za ukanda huo wa Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati zikiwemo Misri, Algeria, Morocco, Libya, Tunisia, Lebanon, Syria, Israel, Iraq na Yemen yanatoka nje ya nchi husika.