Maambukizi mapya ya Ukimwi yapungua: UNAIDS

29 Novemba 2013

Wakati dunia inaelekea kuadhimisha siku ya Ukimwi duniani tarehe Mosi Disemba, habari njema ni kwamba idadi ya maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha Ukimwi imepungua. Taarifa hizo zimo kwenye ujumbe wa siku hiyo uliotolewa na mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya Ukimwi, UNAIDS Michel Sidibé. Katika ujumbe huo wa video, Sidibé anasema..

Idadi ya maambukizi mapya ya HIV imepungua, Idadi ya vifo vitokanavyo na Ukimwi imepungua, Idadi ya watu wanaopata dawa ya kupunguza makali ya Ukimwi imeongezeka. Kwa mara ya kwanza tunaweza kuona mwisho wa janga ambalo limeleta uharibifu mkubwa duniani.”

Bwana Sidibé amesema kutokomezwa kwa Ukimwi kutamaanisha kusherehekea siku za kuzaliwa badala ya kuhudhuria mazishi lakini akaonya..

“Tusilaghaike! Unyanyapaa, kutokukubali na kuridhika kunaweza kuzuia njia yetu. Tuunganishe jitihada na sauti zetu! Mwisho wa Ukimwi uko ndani ya uwezo wetu.”