Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Awamu ya pili ya uchaguzi Mali Jumapili, MINUSMA kutoa usaidizi

Awamu ya pili ya uchaguzi Mali Jumapili, MINUSMA kutoa usaidizi

Wakati raia wa Mali Jumapili ya tarehe 11 mwezi huu watapiga kura katika awamu ya pili ya uchaguzi wa Rais, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuweka utulivu nchini humo, MINUSMA imesema inasaidia mamlaka za Taifa za uchaguzi kusambaza vifaa kwenye maeneo ya ndani zaidi Kaskazini mwa nchi. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani ya kwamba MINUSMA inapeleka vifaa muhimu kwenye maeneo ya Timbuktu, Gao, Kidal na Mopti tayari kwa awamu ya pili ya uchaguzi kama ilivyofanya awamu ya kwanza tarehe 28 mwezi uliopita ambapo hakuna mshindi aliyepata idadi ya kura inayotakiwa kutangazwa mshindi. Amesema MINUSMA pamoja na kusaidia ulinzi na usalama, pia inaandaa ndege ya kuelekea Nema, Mauritania ili kuhakikisha raia wa Mali wanaoishi ukimbizini nchini humo wanaweza kupata kadi za kupigia kura, ikiwa ni jitihada za Umoja wa Mataifa kuhakikisha wakimbizi waliojiandikisha wanapiga kura.