Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 50 ya Umoja wa Afrika umeshuhudia mafanikio: Ban

Miaka 50 ya Umoja wa Afrika umeshuhudia mafanikio: Ban

Umoja wa Mataifa unajivunia kuendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika na wakazi wa bara hilo katika kuweka mazingira ya fursa na matumaini kwa wote, ni ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon hii leo tarehe 25 Mei, ambapo Umoja wa Afrika uliotokana na Umoja wa nchi huru za Afrika, OAU unatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.  Amesema wakati waafrika wanakumbuka waasisi na magwiji wa karne ya 20 waliojitolea kwa hali na mali kupigania ukombozi na Umoja, ni wakati muhimu pia kuwa na matarajio ya zama za ustawi na amani.  Bwana Ban amesema sherehe za kuanzishwa OAU mwaka huu ni za kipekee kwa kuwa zinaangazia miaka Hamsini na kwamba muongo uliopita umeshuhudia mafanikio mengi barani Afrika ikiwemo kuanzishwa kwa mpango mpya wa maendeleo kwa bara hilo, NEPAD pamoja na mpango wa kujitathmini masuala ya utawala bora, APRM. Hata hivyo amesema bado kuna changamoto zilizogubika barahiloakizitaja baadhi kuwa ni mizozo, uharibifu wa mazingira na miundombinu. Amesema ni lazima kusongesha jitihada za kufikia malengo ya maendeleo ya milenia, kuanzia yale ya afya ya wajawazito hadi Ukimwi na kuweka ajenda ya ustawi wa Afrika katika mjadala wa maendeleo baada ya mwaka 2015.