Ban ahitimisha ziara Msumbiji

21 Mei 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amehitimisha ziara yake nchini Msumbiji, huku akiisifu nchi hiyo kwa hatua ilizopiga kimaendeleo. Mengi zaidi na Joshua Mmali

TAARIFA YA JOSHUA MMALI

Akihitimisha ziara yake nchini Msumbiji, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema katika kipindi cha miongo miwili ilopita, nchi hiyo imepiga hatua, na kuonyesha kuwa nchi inaweza kujikwamua kutoka katika mizozo. Amesema tangu kutiwa saini mkataba wa amani mnamo mwaka 1992, Msumbiji imekuwa ikipiga hatua kuelekea kwa demokrasia ya kina, maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na utulivu wa kisiasa.

Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari, ambao pia ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, Bwana Ban ametangaza kuwa amemteua Rais Guebuza kuwa mjumbe bingwa wa elimu.

“Msumbiji imepiga hatua katika kuendeleza elimu na usawa wa kijinsia. Asubuhi ya leo, nikikutana na Rais Gebuza, nikisifu hatua zilizopigwa katika elimu, nimemwomba Rais Gebuza achukue wajibu wa kuwa mjumbe bingwa wa elimu, na nimefurahi kuwa amekubali wajibu huo wa kuwa mjumbe bingwa wa elimu.”

Bwana Ban pia ameisifu Msumbiji kwa mchango wake katika juhudi za maendeleo ya kikanda, pamoja na kugusia ziara anayaonuia kufanya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC na jinsi anavyotarajia kuwahusisha viongozi wengi zaidi katika kuutatua mzozo mashariki mwa DRC, wakati wa mkutano wa Muungano wa nchi za Afrika mjini Addis Ababa.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter