Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru yaanza kurejea Somalia

Nuru yaanza kurejea Somalia

Nchini Somalia hususan mji mkuu Mogadishu ambapo awali vikundi vya kigaidi vilitamba, hali ya amani imeanza kutengamaa. Wananchi nyakati za usiku wanafanya shughuli zao hata kucheza mpira wa miguu ambao awali ulipigwa marufuku na Al Shabaab. Je nini imesababisha hali hii? Jiunge na Assumpta Massoi kwa ripoti maalum…

Mji Mkuu wa Somalia, Mogadishu, giza limeingia…..kwa miaka kadhaa, nyakati kama hizi zilikuwa ni za hofu na mashaka kwa wakazi wa mji huu na maeneo mengine ya nchi juu ya usalama wao. Wengi walishuhudia jua likizama huku hofu ikitanda kutokana na kitisho cha kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab ambacho kwao giza lilikuwa ni fursa ya kutekeleza mashambulizi.

Hata hivyo miezi 18 iliyopita kikundi hicho kilipoteza ngome yake kwenye kitovu cha Somalia baada ya jeshi la ulinzi la kitaifa kuimarika kutokana na msaada wa kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, AMISOM.

Hatua hizo unazozikia ni za askari aw kikosi maalum cha polisi cha AMISOM ambao hapa wanatia shime kikosi cha polisi cha Somalia, SPF wakati wanafanya kazi yao ya kurejesha utawala wa kisheria kwenye mji wa Mogadishu, mji mkubwa zaidi nchini Somalia ambao kwa miongo miwili umeshuhudia mapigano kati ya wakazi wake.

Wakazi wa mji huu wanasema usumbufu wowote wanaopata wakati SPF wako katika doria, si kitu kwa kuzingatia kuimarika kwa usalama kwa miezi ya hivi karibuni. Miongoni mwa wakazi hao ni Jamma Mohammed, raia wa kisomali aliyerejea nchini mwake baada ya amani kutengamaa.

(SAUTI YA JAMMA)

Hakuna tatizo. Kama unafanya kazi, lazima kazi hiyo ikamilike, kwa hiyo usalama ninaoshuhudia sasa naona nafuu usiku kwa hiyo sioni tatizo."

Licha ya kundi la Al Shabaab kujitoa Mogadishu mwezi Agosti mwaka 2011, kundi hilo lenye uhusiano na Al Qaeda limekuwa likifanya mashambulizi ya hapa na pale mjini humo. Hata hivyo mafunzo na msaada wa askari kuoka kwa askari polisi wa kikosi cha AMISON kutoka Uganda na Nigeria, SPF inajivunia kuwa na uwezo wa kuendesha doria thabiti kwenye mitaa ya Mogadishu. Meja Abdi Mohammed Abdille ni Kamanda wa SPF:

(SAUTI Abdi)

Unaweza kuona mabadilko ambapo askari wetu wako mtaani usiku wakiwa na sare. Awali jua lilipozama walikuwa wanaficha sare zao. Amani haikuwepo. Kwa sasa tunakagua magari, nyumba na tunapata vitu kadhaa. Ni mabadiliko ya dhati."

Usiku huu, doria ya pamoja inafanyika kwenye mtaa ambako vijana wanacheza mpira wa miguu sehemu ya uwazi chini ya mbalamwezi. Hii ni dalili kuwa mambo yamebadilika mjini Mogadishu. Kuna wakati Al Shabaab ilipiga marufuku mpira wa miguu. Ni wakati murua kwa SPF na washirika wako AMISOM ambao huwa na saa sita za pamoja usiku wakifanya doria. Ikenna Ikere, Kamanda wa AMISOM kutoka Nigeria

(SAUTI Ikenna)

Wataenda maeneo hatarishi iwapo wataona mtu yeyote wanamkamata. Katika makutano yoyote ambayo ni hatarishi watasimama na kufanya ukaguzi na baada ya hapo tunaendelea na doria."

SPF bado ina safari ndefu kabla ya kuweza kufanya kazi yenyewe, na AMISOM imejizatiti kusaidia kwa kuwapatia mafunzo na msaada zaidi unahitajika wa vifaa, silaha,a magari na mengineyo.

Hata hivyo usiku huuu, kuna fursa ya kucheza dansi kidogo mtaani, kabla doria haijaendelea kwa sababu safari ya amani na utulivu wa kudumu nchini Somali ndio imeanza kwa dhati.

Naam ni kiashiria kwamba sasa amani inashika kasi. Asante Assumpta kwa ripoti hiyo na kwako msikilizaji kwa kujumuika nasi. Basi hadi wakati mwingine kwa ripoti nyingine mimi ni Alice Wairimu Kairuki, kwaheri kwa sasa.