Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akiutazama mwaka 2010 Ban amesema umekuwa wa kishindo kwa UM

Akiutazama mwaka 2010 Ban amesema umekuwa wa kishindo kwa UM

Katika mkutano wake wa mwisho wa mwaka na waandishi wa habari hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema 2010 umekuwa mwaka wa kishindo kwa Umoja wa Mataifa.

Amesema kuna hatua zimepigwa kwenye masuala kama ya bayo-anuai, kusaidia uchaguzi Iraq na Aghanistan, lakini akaonya kwamba bado kuna changamoto kubwa mbele kama suala la Sudan, Mashariki ya Kati na matatizo mengine yanayoikabili dunia.

Kwa kuganga yajayo Ban amesema changamoto iliyopo ni kusukuma mbele mchakato wa mafanikio kwa ajenda ya 2011 ambaye amesema ataitanabaisha kwa kina mwezi ujao, hasa kwa kuzingatia kwamba masuala ya fedha ni magumu huku mahitaji ya Umoja wa Mataifa yakiongezeka.

Ameongeza kuwa hili linahitaji sote kujikita katika kuzuia, maandalizi, kuwa makini na wastahimilivu, yote haya yakiambatana na mfumo wa uwazi na uwajibikaji. Kuhusu Mashariki ya Kati kwa mara nyingine ameitaka Israel na Palestina kushiriki kikamilifu katikia mchakato wa amani na , ameiomba tena Israel kusitisha ujenzi wa makazi ya Walowezi ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki.

Kwa upende wa Myanmar licha ya dosari amesema uchaguzi mkuu, na kuachiliwa kwa Daw Aung San Suu Kyi ni maendeleo makubwa nchini humo. Kwa siku zijazo amesema UM utaongeza juhudi za kupata suluhu ya muda mrefu kwa masuala ya amani ya Korea, mipango ya nyuklia ya Iran, kuleta serikali ya kudumu Somalia na kuleta utengamano katika ya Wacyprus wa asili ya Uturuki na wale wa asili ya Ugiriki.

Kwa Haiti ameelezea hofu yake juu ya madai ya udanganyifu kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi na kuahidi kuendelea kuisaidia nchi hiyo. Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kwenye malengo ya maendeleo ya milenia, msaada wa dola bilioni 40 uliochangishwa, kuanzishwa kwa chombo kipya cha kushughulikia masuala ya wanawake, hatua iliyofikiwa Nagoya Japan, na Cancun Mexico katika mabadiliko ya hali ya hewa na kupunguza gesi chafu.