Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwezi Mtufuku, amani na maridhiano vitamalaki Libya badala ya vurugu: UNSMIL

Mwezi Mtufuku, amani na maridhiano vitamalaki Libya badala ya vurugu: UNSMIL

Mkutano baina ya viongozi wa kisiasa na wanaharakati nchini Libya umefanyika huko Algeria hii leo ambapo Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Libya Bernardino Leon amesema umefanyika katika kipindi muhimu cha kuamua mustakhbali wa nchi hiyo.

Amesema ni kipindi muhimu kwa kuwa washiriki wana fursa ya kuchagua iwapo wako tayari kufikia makubaliano baada ya mapendekezo ya muda mrefu ya kufanyika mwa mkutano huo au wakubaliane kuwa hawawezi kufikia muafaka na hivyo Libya iendelee na vita.

Hata hivyo amesema kupitia maoni ya baadhi ya washiriki na wananchi wa Libya, suala la vita halina fursa hivyo mkutano wa sasa ni fursa ya kuweka historia ya kujenga amani kwa kuzingatia mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhani unakaribia ambao ni msimu wa maridhiano na amani.

Kwa mantiki hiyo Leon ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL ametaka wakati wa mfungo, uwe msimu wa amani na maridhiano, mkusanyiko wa familia uchukue nafasi ya mapigano na mizozano.