Skip to main content

Baraza la Usalama latoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini.

Baraza la Usalama latoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini.

Wanachama wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameeleza wasiwasi wao mkubwa kuhusu hali ya usalama na kibinadamu nchini Sudan Kusini, wakikariri uungwaji mkono wao kwa uongozi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS katika kutimiza wajibu wake na kulinda raia.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Baraza hilo baada ya uamuzi wa serikali ya Sudan Kusini wa tarehe 29, Mei, kumfukuza Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Toby Lanzer.

Wanachama wa Baraza la Usalama wamesema kwamba uamuzi huo unaonyesha kuwa serikali ya Sudan Kusini haijali kabisa hatma ya raia wake wakati huu ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limetangaza kuwa Sudan Kusini inakabiliana na hatua ya juu kabisa kihistoria ya ukosefu wa uhakika wa chakula, jamii ya kimataifa ikijaribu kufikisha usaidizi kwa raia hawa.

Aidha wawakilishi hao wamelaani vikali ukiukaji wa sitisho la mapigano la Januari, 2014, pamoja na mashambulizi yaliyotokea ndani ya kambi ya UNMISS, mjini Malakal, tarehe 28, Mei, ambapo watu wanne wameuawa, wakiisihi serikali ya Sudan Kusini kuchukua hatua mara moja ili kuhakikisha usalama wa raia na wa kambi za UNMISS.

Halikadhalika wanachama wa baraza hilo wameziomba pande zote kuwezesha UNMISS kutekeleza majukumu yake na kusitisha matishio dhidi ya ujumbe huo, hatimaye wakiziomba kushirikiana kwa dhati kwenye utaratibu wa amani ili kupata suluhu ya kisiasa kwa mzozo huu.