Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 15 wahanga wa ukatili vitani mwaka 2014:

Watoto milioni 15 wahanga wa ukatili vitani mwaka 2014:

Baraza la Usalama leo limekuwa na mjadala maalum kuhusu watoto walio wahanga wa vikundi vilivyojihami, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akisema mwaka 2014 umekuwa mwaka mbaya zaidi kwa usalama wa watoto, milioni 15 wakiwa wahanga wa ukatili huo. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Akihutubia Baraza la Usalama, Ban amesema watoto milioni 230 walikuwa wanaishi kwenye maeneo ya mapigano mwaka 2014 akisema kwamba wamezidi kulengwa na vikundi vilivyojihami.

Ametaja mfano wa Iraq, Syria au Nigeria, ambapo idadi ya matukio ya utekaji nyara, ukatili wa kijinsia, utumikishwaji wa watoto vitani, na mashambulizi dhidi ya shule yameongezeka zaidi mwaka jana.

(Sauti ya Ban)

“ Ongezeko la msimamo mkali wa dini katika maeneo ya vita linatia wasiwasi sana . Mikakati ya vikundi kama Daesh au Boko Haram haitofautishi raia na jeshi. Vikundi hivi si vitisho kwa usalama wa kimataifa tu lakini pia kwa watoto wanaolengwa” .

Naye mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu watoto vitani, Leila Zerrougui, ambaye mwaka jana alianzisha kampeni ya watoto si jeshi akasema..

(Sauti ya Zerrougui)

"Ni vigumu sana kwangu kutambua kwamba bado tunakumbwa kila mwaka na changamoto mpya, licha ya makubaliano ya wote na jitihada zetu kuzuia watoto kupitia mateso ya vita. Mwanzo wa mwaka huu wa 2015, ukatili wa vikundi vilivyojihami na ukatili wanaowafanyia watoto ni changamoto yetu ya kwanza. Ni hivyo Iraq, Syria na Nigeria lakini pia katika nchi zingine”

Hatimaye wanachama wa Baraza la Usalama walisikiliza maoni ya mtoto aliyetumikishwa na waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Junior Nzita Nsuami, ambaye sasa hivi anajaribu kuelimisha wenzake.