Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake watumwa walikuwa jasiri licha ya madhila: Ban

Wanawake watumwa walikuwa jasiri licha ya madhila: Ban

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kumbukizi ya wahanga wa utumwa na biashara ya utumwa kupitia bahari ya Atlantiki, Umoja wa Mataifa umeamua kutumia siku hiyo kukumbuka wanawake wengi watumwa waliosimama kidete kutetea utu wa jamii zao licha ya madhila yaliyokuwa yanawapata.Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-moon katika ujumbe wake wa siku hiyo amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa mchango wao jasiri wa kuhakikisha wanasimamia utu mara nyingi unasahaulika.

Amesema wanawake hao walikuwa mstari wa mbele kupinga madhila waliyokabiliana nayo kama vile utumikishwaji wa kingono, kulazimishwa kuzaa watoto na hata kuuza watoto wao.

Ban amesema ingawa biashara hiyo ilifanyika kwa zaidi ya karne nne kuanzia karne ya 16, misingi yake  ambayo ni ubaguzi, bado imejikita katika jamii na kuwezesha utumwa wa zama za sasa.

Ametolea mfano ajira za lazima, utumikishaji wa kingono na usafirishaji haramu.

Kwa mantiki hiyo ametaka kurejelewa kwa ahadi ya kutokomeza aina za kisasa za utumwa ili watoto waweze kuishi kwenye dunia yenye fursa sawa kwa wote bila aina zozote za ubaguzi.

Katika kumbukizi ya siku hii Katibu Mkuu atazindua katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kumbukizi ya kudumu ya wahanga wa utumwa na biashara ya utumwa kupitia bahari ya Atlantiki.

Lengo la kumbukizi hiyo ni iitwayo Safina ya marejeo ni kusaidia kuponya makovu ya utumwa wakati wahanga wanapokumbukwa.