Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya dunia yarejesha operesheni zake Guinea Bissau

Benki ya dunia yarejesha operesheni zake Guinea Bissau

Benki ya dunia imetangaza kuanza tena kwa operesheni zake nchini Guinea Bissau baada ya kusitisha kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwezi Aprili mwaka 2012.

Tangazo hilo limetolewa wakati wa mjadala wa bodi tendaji ya Benki hiyo kuhusu hatma ya uhusiano kati yake na nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya dunia nchini Guinea Bissau Vera Songwe amesema urejeshaji wa uhusiano unalenga kuweka misingi ya amani endelevu na kasi ya maendeleo kwa kuipatia msaada muhimu kwa kipindi cha miaka miwili ijayo baada ya nchi hiyo kujikwamua kutoka kwenye mzozo.

Mathalani usaidizi ni katika kuwezesha serikali kujenga taasisi muhimu, kuimarisha sekta ya umma na kurejesha huduma za msingi.

Benki ya dunia inasema Guinea Bissau ni moja ya nchi chache za Afrika ambako umaskini umetwama au umeongezeka katika kipindi cha miaka michache iliyopita.