Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna vikwazo vya usafiri Afrika Magharibi licha ya kuenea kwa kirusi cha Ebola- WHO

WHO/T. Jasarevic
Photo: WHO/T. Jasarevic

Hakuna vikwazo vya usafiri Afrika Magharibi licha ya kuenea kwa kirusi cha Ebola- WHO

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa hatari ya wasafiri wa ndege kueneza maambukizi ya kirusi cha Ebola kutoka nchi zilizoathiriwa bado  ni ndogo, lakini haiwezi kupuuzwa. Taarifa kamili na Amina Hassan.

Taarifa ya Amina

WHO haijapendekeza vikwazo vyovyote vya usafiri hadi sasa au kufungwa kwa mipaka kwa sababu ya mlipuko wa Ebola, ingawa imetoa wito kwa mamlaka za afya na kampuni za ndege zinazosafiri kutoka nchi zilizoathiriwa kuwa makini zaidi.

Shirika hilo la afya limesema kuwa mlipuko wa Ebola Guinea, Liberia na Sierra Leone bado ni hatarishi, huku maambukizi yakiendelea katika jamii na vituo vya afya. Kufikia sasa, zaidi ya watu 729 wamepoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Liberia na Sierra Leone zimetangaza hali ya hatari ya afya ya umma, na kuwazuia watu katika maeneo yaliyoathirika zaidi kutoka nje.

Gregory Hartl ni msemaji wa WHO mjini Geneva.

“Hatari ya mtu aliyeathiriwa tayari na Ebola kusafiri kwa ndege ipo chini mno. Unatakiwa kumgusa mtu ambaye tayari anaonekana ni mgonjwa, au kugusa unyevunyevu wa mwili wake ili uambukizwe. Ukimgusa mtu unaugua haraka sana, kwa hiyo tunadhani hatari ya kuwepo visa vya vya maambukizi kupitia angani ni adimu, ingawa kinaweza kutokea. WHO imekuwa ikiwasiliana na Shirika la Safari za Anga, ICAO na IATA, na wanazingatia masuala haya, na tutatoa ushauri zaidi kuhusu usafiri wa angani karibuni”

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Margaret Chan yupo Afrika ya Magharibi, ambako anatarajia kukutana na viongozi wa nchi zilizoathiriwa kesho Ijumaa, ili kutathmini mipango iliyopo ya kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo hatari.