Kutokomeza njaa kuende sambamba na kukabili mabadiliko ya hali ya hewa: Figueres
Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya chakula duniani katibu mtendaji wa mpango wa mkutano wa Umoja wa mataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa UNFCCC Chriatiana Figueres amesema usalama wa chakula na mabadiliko ya tabia nchi vinahusiana. Siku ya kimataifa ya chakula inaadhimishwa kila mwaka Oktoba 16 tangu mwaka 1945 lakini mamilioni ya watu hawapati chakula cha kutosha au wanakabiliwa na matatizo ya chakula na mabadiliko ya hali ya hewa yanazidisha changamoto katika kuilisha idadi ya watu inayoongezeka kwa kasi. Mbali ya hali ya kudumu inayobadilikabadilika ambayo itaathiri kilimo , mabadiliko ya tabia nchi yanasababisha hali mbaya ya hewa mfano vimbunga, mafuriko na ukame uliokithiri , hali ambazo zinaweza kuwafanya wakulima na watu wengine wanaoishi katika hali hizo kuwa upungufu wa chakula na matatizo makubwa. Bi figueres amesema endapo dunia inataka kuendelea kulisha idadi ya watu inayoongezeka katika siku za usoni basi inahitaji kuchukua hatua leo ambazo zitawaandaa wakulima duniani kote kwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Ameongeza kuwa hatua tayari zimechukuliwa lakini kinachohitajika ni kuziongeza zaidi.