Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM yanuia kukomesha karaha ya utumiaji mabavu dhidi ya wanawake

UM yanuia kukomesha karaha ya utumiaji mabavu dhidi ya wanawake

KM wa UM Ban Ki-moon aliwasilisha risala maalumu, na muhimu, kwenye taadhima za kuiheshimu Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumiaji Mabavu dhidi ya Wanawake. Jumuiya ya Kimataifa iliafikiana kuitambua tarehe 25 Novemba, kila mwaka, kuwa ni siku kuuzindua umma wa dunia juu ya jukumu kuu, na tukufu, la kupiga vita, kipamoja, vitendo karaha vya kutumia mabavu na nguvu dhidi ya watoto wa kike na wanawake.

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu Duniani, Louise Arbour naye pia aliunga mkono fafanuzi hizo za KM. Alisisitiza kwenye risala yake ya kuiheshimu Siku ya Kukomesha Utumiaji Mabavu dhidi ya Wanawake kwamba jamii ya kimataifa itahitaji kubuni sheria imara mpya, zitakazokuwa na uzito wa kimataifa, ili kutumiwa katika juhudi za kuwakinga wanawake na mateso ya wale wenye kutumia nguvu dhidi yao, mateso ambayo, alitilia mkazo, hukiuka maadili ya kiutu na haki halali za kibinadamu. Bi Arbour alikumbusha ya kuwa “kila siku, idadi isiohisabika ya watoto wa kike na wanawake, katika pembe mbalimbali za dunia, huuliwa, hulemazwa na hupigwa, na mara nyengine hunajisiwa kimabavu, na vile vile huchuuzwa na kufanywa watumwa wa kijinsia na kuteswa kihorera.” Kamishna wa UM juu ya Haki za Binadamu alionya kwamba mateso haya yote hutukia kwa sababu ya upungufu wa sheria madhubuti, za kimataifa na kitaifa, za kuadhibu kama inavyopaswa wale wenye kutesa, kunyanyasa na kudhalilisha wanawake. Alisema kunahitajika sheria zinazoaminika na kutegemewa na waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia. Chanzo cha udhalilishaji wa wanawake, alionya Arbour, kinatokana na “ubaguzi wa kijinsia ikichanganyika na ukosefu wa usawa wa kisheria.” Kwa hivyo, aliitaka jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kunakuwepo usawa wa kijinsia kwenye huduma za kiuchumi na kijamii kwenye maeneo yao, hatua ambayo ikikamilishwa anaamini itasaidia pakubwa kusitisha udhalilishaji wa wanawake kote duniani.

KM Ban na Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu wamekumbusha kwenye risala zao kwamba udhalilishaji na unyanyasaji wa watoto wa kike na wanawake, ni makosa ya dhulma na ukatili wenye kutengua kihakika sheria zote za kiutu na ubinadamu.