Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano

Umuhimu wa familia katika jamii nchini Kenya

Siku ya familia duniani imekuewa ikiadhimishwa  Mei  15 kila mwaka tangu ipitishwe na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1993. Lengo ni kutoa fursa ya kuchagiza uelewa kuhusu taasisi hiyo muhimu kabisa ili kuimarisha maarifa kuhusu maswala ya kijamii, kiuchumi na mabadiliko yanayoathiri familia.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya je wanaume wanawajibika? Inalenga kuimarisha usawa wa kijinsia na haki za watoto katika familia. Aidha unapigia chepuo kuzuia ukatili katika familia kupitia sheria na mikakati na programu za kuingilia kati.

Wakimbizi wa Burundi wamiminika Rwanda

Wakati mzozo wa kisiasa nchini Burundi ukiendelea,  wananchi wasio na raia wanateseka ambapo maelfu kwa maelfu wamekimbilia nchi jirani  kusaka hifadhi ikiwamo Rwanda na Tanzania.Wakimbizi hawa hukumbana na madhila mbalimbali katika harakati za kusaka hifadhi kama anavyosimulia Joseph Msami katika makala ifuatayo.

Shamrashamra Liberia baada ya Ebola kudhibitiwa

Baada ya mwaka mzima wa kuishi na janga la Ebola na kusaka mbinu ya kuondokana na jinamizi hilo, hatimaye sasa Liberia iko huru kwani imetangazwa rasmi kutokuwa na maambukizi mapya ya kirusi hicho hatari. Shughuli zinarejea katika hali ya kawaida na wiki hii imeshuhudia mojawapo ya shughuli maalum ya ufunguzi wa shule ya sekondari ya kati na juu mjini Monrovia. Mamia ya watu walijitokeza katika tukio hilo kama anavyosimulia Assumpta Massoi kwenye makala hii.

Viongozi na watendaji wakuu serikalini wana wajibu kulinda misitu Afrika

Wakati kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu misitu, likiingia wiki ya pili jijini New York, Marekani,  washiriki wa kongamano hilo wanatarajiwa kufikia makubaliano ya kimataifa kuhusu misitu. Miongoni mwa washiriki  ni Godwin Kowero ambaye ni mkurugenzi shirika la misitu la African Forestry Forum lenye makao yake makuu mjini Nairobi Kenya. Kwa upande wake akiwa  mwakilishi kutoka Afrika anasema kwamba bara hilo lina ujumbe mahsusi ambao unaendana na ajenda nzima ya mkutano ambapo katika mahojiano na Grace Kaneiya wa Idhaa hii anaanza kwa kueleza ujumbe huo.

Harakati za kukabiliana na ugonjwa wa fistula nchini Kenya

Huku Vifo vya wanawake wajawazito wakati wa kujifungua vikisalia kuwa tatizo kuu, Kenya inakabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa fistula, ambao hutokea mama anapojifungua baada ya uchungu wa muda mrefu na kuchanika kutoka sehemu ya haja ndogo hadi haja kubwa.Kulingana na Shirika la Umoja la idadi ya watu duniani UNFPA, kati ya visa 3000 vya Fistula ambavyo vinatokea kila mwaka nchini humo, ni asilimia 7 tu ya wanawake wanapata huduma za matibabu. Katika makala hii ya Joseph Msami,  wanawake wazungumzia madhila waliyokumbana nayo baada ya kuugua Fistula.

Miradi yaleta nuru miongoni mwa jamii za wasamburu nchini Kenya

Nchini Kenya jamii za wafugaji zinakabiliana na changamoto mbali mbali ikiwemo malisho ya mifugo yao wakati huu ambapo idadi ya watu na mifugo inaongezeka, na mabadiliko ya tabianchi yanaathiri upatikanaji wa mahitaji ya makundi hayo.

Mathalani miongoni mwa jamii za wasamburu, changamoto hizo ziko dhahiri lakini miradi iliyoanzishwa sasa inaleta nuru.

Jeni nini kinafanyika? Ungana na Grace Kaneiya kwenye makala hii.

Mazingira ya kazi uliko yako salama?

Wakati siku ya kimataifa ya usalama na afya makazini ikiadhimishwa wiki hii  , Shirika la Kazi Duniani(ILO) limetoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zifanye kazi kwa bidii kuimarisha usalama na afya katika maeneo ya kazi.

Tamko la ILO kwa nchi wanachama linamnukuu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Guy Ryder akisema kuwa sababu za kiuchumi au msukumo wa kupata faida hauwezi kuachiwa uruhusu kupindisha taratibu za kazi na hivyo kuathiri maisha ya mamilioni ya wafanyakazi duniani kupitia vifo, majeruhi au magonjwa kazini.