Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Guterres asikitishwa na shambulio la New York

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres ameelezea kusikitishwa na kutiwa hofu na shambulio llilofanyika jijini New York Marekani Jumanne, katika mji ambao ndiko  makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Guterres ametuma salamu zake za rambi rambi kwa familia za wahanga na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi.

Umeme wasalia ndoto kwa wakazi wengi Afrika – Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesihi serikali zichukue hatua kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya nishati salama iwe ya kupikia au ya kuangazia mwanga.

Bwana Guterres amesema hayo leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakati akihutubia warsha kuhusu ushirikiano wa matumizi ya nishati duniani kwa lengo la kusongesha maendeleo endelevu.

Amesema hivi sasa watu bilioni moja duniani hawana kabisa huduma ya umeme ambapo milioni 500 wako Afrika na waliosalia wako ukanda wa Asia na Pasifiki.

WHO na MONUSCO wasaidia wahanga wa kipindupindu DRC

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, shirika la afya ulimwenguni WHO na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO wamewasilisha dawa kwa wahanga wa mlipuko wa ugonjwa kipindupindu kwenye eneo la Walikale, jimbo la Kivu Kaskazini, ugonjwa ambao umesababisha vifo vya watu 29 ndani ya wiki tatu.

Usaidizi huo unaofuatia ombi kutoka serikali ya jimbo hilo ni pamoja na kilo 700 za dawa kwa ajili ya wagonjwa kwenye kitongoji cha Oninga kilichopo kilometa takribani 300 kutoka mji wa Walikale.