Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

FAO yaleta unafuu kwa wanawake wanaofuga kuku Gambia

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema miradi yake katika nchi za Afrika imeanza kukwamua wanawake wajasiriamali kwa kuwawezesha kuinua vipato na wakati huo huo kuhakikisha upatikanaji wa chakula.

Afisa mwandamizi FAO anayehusika na usawa wa kijinsia na maendeleo vijijini Thacko Ndiaye amesema hayo katika mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ambako anahudhuria mkutano wa 61 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW61.

Maarifa ni sehemu kubwa ya ukuaji wa uchumi duniani-WIPO

Shughuli za uchumi kote duniani zina kipengee muhimu cha maarifa kuliko wakati mwingine wowote, kwa mujibu wa takwimu za karibuni zilizotolewa na shirika la kimataifa la hati miliki (WIPO).

Katika Ripoti yake kwa mwaka 2016 shirika hilo linasema limeshuhudia idadi kubwa ya maombi ya kimataifa ya kulinda masuala ya ubunifu, nembo za biashara na mitindo ya viwandani. Miongoni mwa nchi zilizotuma maombi mengi ni Japan, Uchina, Ujerumani na Jamhuri ya watu wa Korea. WIPO ni jukwaa la kimataifa kwa ajili ya huduma za hati miliki, sera , taarifa na ushirikiano.

Somalia yaanza kutoa chanjo dhidi ya Kipindupindu

Serikali ya Somalia kwa usaidizi wa shirika la afya duniani, WHO limeanza kutoka chanjo dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kwa watu zaidi ya 450,000 nchini humo.

Mwakilishi wa WHO nchini Somalia Dkt. Ghulam Popal amesema watoto wenye umri wa kuanzia miaka miwili hadi watu wazima watapatiwa chanjo hiyo ya matone kwa awamu mbili kwenye maeneo ya Mogadishu, Kismayo na Beledweyne ambayo yako hatarini zaidi.

Hii ni mara ya kwanza kwa aina hiyo ya chanjo kutolewa nchini Somalia wakati huu ambapo kipindupindu kimesababisha vifo vya watu 268 tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2017.

Uwakilishi wa wanawake kwenye serikali na bunge wadorora- IPU

Idadi ya wanawake walioko kwenye serikali na mabunge kote duniani inadorora licha ya matumaini kuwepo mwaka 2015.

Hiyo ni kwa mujibu wa ramani mpya kuhusu wanawake katika siasa mwaka 2017 iliyozinduliwa hii leo jijini New York, Marekani na umoja wa mabunge duniani, IPU na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya wanawake, UNWomen kando mwa kikao cha kamisheni ya hali ya wanawake.

Mathalani idadi ya wanawake marais au wakuu wa serikali imeshuka kutoka 19 mwaka 2015 hadi 17 mwaka huu.

Yemen yahitaji msaada wa dharura wa chakula- FAO

Uhaba mkubwa wa chakula unatishia uhai wa zaidi ya watu milioni 17 nchini Yemen ambako mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanaendelea kushika kasi tangu mwaka 2015.

Taarifa hizo zimo kwenye ripoti ya uchambuzi kuhusu uhakika wa chakula nchini humo, ripoti iliyochapishwa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake wa misaada ya kibinadamu.

Mathalani imesema uhaba mkubwa wa chakula ni  katika majimbo 22 huku theluthi mbili ya wananchi wakihitaji msaada wa chakula ili kuokoa maisha yao hali ikiripotiwa kuwa mbaya zaidi kwenye majimbo ya Taiz na Al Hudaydah.

Ni wakati wa malipo sawa kwa wanaume na wanawake:UN Women

Patricia Arquette nyota wa Marekani wa kucheza filamu amekuwa miongoni mwa wanaharakati mashuhuri waliotoa wito katika kikao cha 61 ya kamisheni ya hali ya wanawake duniani wa kumaliza tofauti za kijinsia imataifa na kuziba pengo la malipo baina ya wanaume na wanawake. Kikao hicho kilichofunguliwa Jumatatu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kitaendelea hadi Machi 24. Bi Arquette akiongoza mjadala huo amesema.

(CLIP YA PATRICIA)

Kilimo cha buni chastawisha maisha ya wanawake Uganda.

Ujasiriamali ni miongoni mwa mikakati bunifu ya kuwawezesha wanawake kuinuka kiuchumi wakati huu ambapo malengo ya maendeleo endelevu SDGs yanapigia chepuo uwezeshaji wa wanawake katika kila ngazi.

Nchini Uganda, licha ya changamoto kadhaa, Betty ni mfano wa wanawake waliofanikiwa kupitia kilimo cha mibuni. Ungana na John Kibego katika makala ya kumulika mafaniko ya mwanamke huyo.

Ulaya na Asia ya Kati zaingia katika mfumo mpya wa utapia mlo:FAO

Ripoti mpya ya shirika la chakula na kilimo FAO inasema Ulaya na Asia ya Kati inaingia katika mfumo mpya wa utapiamlo, ikiainisha ongezeko la utipwatipwa na maradhi mengine yanayoambatana na hali hiyo.

Shirika hilo linasema ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa kipato vimesaidia kuondoa njaa katika kanda hizo lakini pia umesababisha mabadiliko ya mfumo kwa walaji na kusababisha tishio na adha zingine za kiafya.