Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen yahitaji msaada wa dharura wa chakula- FAO

Yemen yahitaji msaada wa dharura wa chakula- FAO

Pakua

Uhaba mkubwa wa chakula unatishia uhai wa zaidi ya watu milioni 17 nchini Yemen ambako mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanaendelea kushika kasi tangu mwaka 2015.

Taarifa hizo zimo kwenye ripoti ya uchambuzi kuhusu uhakika wa chakula nchini humo, ripoti iliyochapishwa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake wa misaada ya kibinadamu.

Mathalani imesema uhaba mkubwa wa chakula ni  katika majimbo 22 huku theluthi mbili ya wananchi wakihitaji msaada wa chakula ili kuokoa maisha yao hali ikiripotiwa kuwa mbaya zaidi kwenye majimbo ya Taiz na Al Hudaydah.

Mwakilishi wa shirika la chakula na kilimo duniani FAO nchini Yemen Salah Hajj Hassan amesema mapigano yanayoendelea yana madhara makubwa katika sekta ya kilimo na watu kujipatia kipato, akisema hata majimbo ya Taiz na Al Hudaydah ambayo huongoza kwa kilimo sasa yamekwama.

Kwa upande wake Stephen Anderson, mwaklishi mkazi wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP amesema kinachohitajika sasa ni usaidizi wa fedha ili kuwapatia chakula pamoja na ruhusa ya kufikishia misaada hiyo bila vikwazo vyovyote.

Photo Credit
Mwanamke na mtoto wake kijijini nchini Yemen. Picha: FAO/Rawan Shaif