Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Licha ya makataba wa amani , machafuko yafurusha maelfu Colombia-UNHCR

Licha ya kusainiwa kwa mkataba wa amani baina ya serikali ya Colombia na kundi la upinzani liitwalo FARC, mwezi Novemba mwaka jana, machafuko nchini humo yanaendelea kufurusha maelfu ya watu, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Mapigano baina ya vikosi hivyo yamedumu kwa miaka 50.

UNHCR licha ya kutambua juhudi za kusaka amani na kuhakikisha haki za wahanga, shirika hilo limeeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa kiwango cha wakimbizi.

Hatari zaidi ya Zika kwa nchi zenye mbu Aedes Aegypti- WHO

Shirika la afya duniani, WHO leo limetoa mwongozo na orodha mpya ya nchi 70 ambazo ziko hatarini kupata maambukizi ya virusi vya Zika.

Mataifa hayo yako katika kanda mbali mbali ikiwemo Ulaya, Amerika, Asia na Afrika ambapo WHO imesema miongoni mwao ni nchi ambako mbu anayeeneza virusi hivyo Aedes Aegypti anapatikana, ingawa maambukizi hayajaripotiwa.

Barani Afrika ni pamoja na Tanzania, Kenya, Rwanda na Malawi ambapo WHO imesema lengo la mwongozo huo si kuzua taharuki bali unalenga kupatia serikali mwelekeo wa kuepusha maambukizi.

Mapigano mapya Yemen yafurusha maelfu ya watu- UNHCR

Mapigano mapya kwenye maeneo ya kati na magharibi mwa Yemen yamelazimisha watu zaidi ya elfu 60 wakimbie makazi yao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema mapigano hayo yanaendelea kwa wiki sita sasa na idadi kubwa ya raia wamekimbilia majimbo ya Taiz na Al-Hudaydah.

Msemaji wa UNHCR William Spindler amesema wananchi hao wanahitaji misaada na sasa wamejihifadhi kwenye maeneo ya umma kama vile shule na vituo vya afya ilhali wengine wanaishi kwenye mahame, watoto wakiripotiwa kuwa na utapiamlo.

(Sauti ya Spindler)

Faida za wahamiaji za kiuchumi zitambulike: UM

Likizingatia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi na wahamiaji wa hivi karibuni, baraza la haki za binadamu hii leo mjini Gweneva Uswisi, limekuwa na mjadala shirikishi kuhusu haki za kundi hilo katika muktadha wa kuhama kwa makundi makubwa.

Wajumbe wa baraza hilo wamesisitiza kuwa kuheshimu haki za binadamu kwa wahamiaji sio tu hitaji la kisheria bali pia ni jambo lenye busara kulitekeleza, wakitolea mfano wa kuwaengua wahamiaji katika mfumo wa afya, elimu na siasa au kuwaeka kizuizini huongeza gharama katika safari yao na nchi watakazofikia.

Usawa hautakamilika iwapo hautajumuisha wanawake mashinani

Ujumuishwaji wa wanawake mashinani ni dhana isiyokwepeka katika kutimizia dhima ya maadhimisho ya siku ya wanawake mwaka huu ambayo ni wanawake katika ulimwengu wa kazi unaobadilika, inayokwenda sambamba na lengo nambari kumi la maendeleo endelevu yaani SDG's, ambalo linachagiza ulimwengu kupunguza ukosefu wa usawa.

Akihojiwa na Idhaa hii, Dkt. Justine Uvuza wa Shirika la asasi za kiraia Landesa ambalo linapigania haki za wanawake masikini na walio mashinani kumiliki ardhi, akisema..

(Sauti Dkt. Uvuza )

Kuna matumaini ya suluhu Burundi, nitaitisha mkutano wa dharura: Mkapa

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo Machi tisa, limejadili hali ya kiusalama nchini Burundi, ambapo imeelezwa kuwa usalama umeendelea kuzorota na hofu imetanda miongoni mwa raia.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuhusu kuzuia migogoro Jamal Benomar, ameliambia baraza hilo kuwa ikiwa ni miaka miwili tangu kuzuka kwa mgogoro nchini humo, uhasama unaendelea miongoni mwa pande kinzani na kwamba.

( Sauti Benomar)

Wagonjwa wa figo Yemen wahaha kupata tiba

Nchini Yemen, mapigano yakiwa yanaendelea kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa Houthi miundombinu ya kiafya inazidi kusambaratika ikiacha wagonjwa taabani wakiwemo wale wa figo.

Shirika la afya ulimwenguni WHO nchini humo linasema kutokana na mapigano, wagonjwa wa figo hivi sasa wanashindwa kupata huduma ya kusafisha damu katika vituo vingine na hivyo kulazimika kwenda jimbo la Al-Hudaydah.

Sitakubali anayepeperusha bendera ya UM atutie aibu- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewasilisha ripoti yake mbele ya Baraza Kuu inayotaja mikakati mipya mahsusi ya kuepusha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kingono kwenye operesheni za ulinzi wa amani za chombo hicho.

Amesema mikakati hiyo ni muhimu kuhakikisha hakuna mtuhumiwa yeyote anakwepa sheria wakati huu ambapo watuhumiwa wa vitendo hivyo mwaka jana pekee ni 145, ambapo 80 kati yao ni walinda amani askari na polisi huku 65 wakiwa ni wafanyakazi wa kiraia wa Umoja wa Mataifa.