Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano mapya Yemen yafurusha maelfu ya watu- UNHCR

Mapigano mapya Yemen yafurusha maelfu ya watu- UNHCR

Pakua

Mapigano mapya kwenye maeneo ya kati na magharibi mwa Yemen yamelazimisha watu zaidi ya elfu 60 wakimbie makazi yao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema mapigano hayo yanaendelea kwa wiki sita sasa na idadi kubwa ya raia wamekimbilia majimbo ya Taiz na Al-Hudaydah.

Msemaji wa UNHCR William Spindler amesema wananchi hao wanahitaji misaada na sasa wamejihifadhi kwenye maeneo ya umma kama vile shule na vituo vya afya ilhali wengine wanaishi kwenye mahame, watoto wakiripotiwa kuwa na utapiamlo.

(Sauti ya Spindler)

“Idadi kubwa ya wakimbizi hao wa ndani wanaokimbia mapigano wanahitaji misaada ya dharura ya chakula, malazi na dawa na pia hawana maji safi na salama na huduma za kujisafi.  Idadi kubwa ya wanawake wanaripotiwa kuwa na usongo wa mawazo na utapiamlo. UNHCR hivi sasa inahamasisha ili kuweza kufikisha misaada kwa wahitaji.”

Kwingineko UNHCR na wadau wake wamechukua hatua haraka kushughulikia mahitaji ya wakimbizi wapya wa ndani Taiz ikiwemo kuwapatia makazi na misaada ya dharura kwa wale wanaowasili kwenye majimbo ya Hudaydah na Ibb.

Misaada hiyo ni pamoja na magodoro, blanketi na vifaa vya kupikia ambapo hadi sasa wamefikia watu zaidi ya elfu 14.

Photo Credit
Raia wa Yemen ambao wamekimbilia majimbo ya Taiz na Al-HudaydahPicha: © UNHCR/Shabia Mantoo