Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

IPU: hatua za kisheria kunyamazisha wabunge zinatia hofu

Muungano wa mabunge IPU, leo Alhamisi umezungumzia ongezeko la kiwango cha ulipizaji kisasi dhidi ya wabunge wanaotumia uhuru wao wa kujileleza kote duniani.

Katika mlolongo wa maamuzi yaliyopitishwa kuhusu haki za binadamu za wabunge , IPU imesisitiza kuhusu ongezeko la hatua za kisheria mahakani na kutimuliwa kwa wabunge katika uwanja wa kisiasa kama njia ya kunyamazisha wapinzani wa kisiasa.

Imeongeza kuwa badala ya kuwasikiliza wapinzani mfumo wa kisheria ndio umekuwa nyenzo ya kuwatupa nje.

Fanyeni maonyesho ya urithi wenu leo-UNESCO

Leo ni siku ya kimataifa ya urithi wa sauti na picha ambapo Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, limesema siku hii inatoa fursa ya kuongeza uelewa wa haja ya kukiri umuhimu wa nyenzo hizi na kuchukua hatua za dharura kuzihifadhi.

Mada kuu ya mwaka huu ni "Ni hadithi yako-usiipoteze", ambapo UNESCO inahimiza ulimwengu wote kusherehekea siku hii kwa kufanya maonyesho ya urithi wa vielelezo vyao kama mpango wa kimataifa wa kukuza thamani yake.

Msumbiji ijipange kukabiliana ukame mwingine- Macharia

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya El Niño na mabadiliko ya tabianchi, Balozi Macharia Kamau, amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaonekana dhahiri nchini Msumbiji ambapo kati ya watu milioni 1.5 na milioni 2.3 wanateseka na ukame ulioletwa na El Niño.

Balozi Kamau ambaye yuko ziarani kwenye ukanda wa Kusini mwa Afrika, amesema matumaini yake ni kujionea mwenyewe hali ilivyo, kuongea na viongozi kudhihirisha mshikamano wa jumuiya ya kimataifa na vile vile kuongeza uelewa wa changamoto zinazoikumba Msumbiji.

Mkimbizi aja na mbinu ya kukabili msongo wa mawazo

Maisha ukimbizini hugubikwa na mambo mengi bila shaka, hofu, athari za kisaikolojia, kutokujua mustakabali, vyote hivi vyaweza kusababisha msongo wa mawazo.

Mkimbizi mmoja nchini Uganda anatumia mbinu mbadala ya kuepuka msongo wa mawazo, na zaidi ya yote huwasaidia wenzako kuhakikisha wanahepa hali hiyo. John Kibego amezungumza naye. Msikilize katika makala hii ya kusisimua.

UM waonya dhidi ya uharibifu wa makusudi wa urithi wa dunia

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za kitamaduni, Karima Bennoune, ametoa wito wa kuchukuliwa haraka hatua za kimataifa dhidi ya uharibifu wa urithi wa utamaduni. Akitoa mifano ya uharibifu huo kwenye kikao cha baraza kuu mjini New York Jumatano, amezitaja nchi za Afghanistan, Iraq, Libya, Mali na kusisitiza kwamba kuna haja ya baraza hilo kuchukulia uharibifu wa utamaduni kama suala la haki za binadamu.

UNHCR mbioni kukabiliana na wimbi la wakimbizi Iraq

Harakati za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR za kupeleka zaidi ya tenti 7,000 katika kambi zitakazohifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wanaotarajiwa kusambaratishwa na mapigano ya Mosul nchini Iraq bado inaendelea.

Akizungumza katika mahojiano na redio ya Umoja wa Mataifa, Bruno Geddo, Afisa wa UNHCR nchini Iraq amesema mji wa Mosul bado una watu zaidi ya milioni 1.2, na shirika hilo linajiandaa kupokea idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani katika kambi tano ambazo ziko tayari kuwapokea na nyingine sita bado zikitayarishwa.

UN Photo.

Vikwazo dhidi ya Cuba; Marekani yachukua hatua ya aina yake

Baada ya kupinga mara 25 azimio la kusaka kuondoa vikwazo vya Marekani vya kiuchumi, kibiashara na kifedha dhidi ya Cuba, hatimaye leo Marekani bada ya kupinga imeamua kutoonyesha msimamo wowote huku nchi 191 zikiunga mkono azimio hilo.

Marekani na Israel mwaka jana zilipinga lakini hii leo azimio likiwasilishwa kwa mara ya 26, kwa pamoja hazikuonyesha msimamo wowote ambapo mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Samantha Power ametaja sababu ya kubadilika kwa msimamo.

(Sauti ya Balozi Power)

UNAMA yalaani mauaji ya raia 26 Ghor:

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA umelaani vikali shambulio lililofanywa na kundi la watu wenye silaha na kukatili maisha ya watu 26 Jumanne kwenye jimbo la Ghor nchini humo.

Watu whao wenye silaha kwa makusudi waliwapiga risasi na kuwauwa wanaume raia kwenye eneo la Ghalmin wilayani Chaghcharan jimbo la Ghor baada ya kuwashikilia mateka watu hao mapema siku hiyo walipokuwa wakisenya kuni kwenye eneo la Firozokh.