Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

India na Ufaransa kuunda setilaiti ya kuchambua tabianchi

India na Ufaransa zitaingia makubaliano ya kuunda setilaiti inayochambua mabadiliko ya tabianchi.

Hatua hiyo inafuatia mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais Francois Hollande wa Ufaransa ambapo taasisi mbili za masuala ya anga za juu za nchi hizo zitahusika na utengenezaji.

Mpango huu unaimarisha ushirikiano wa awali kati ya taasisi hizo za ISRO ya India na CNES ya Ufaransa ambapo tayari walishatengeneza setilaiti mbili za kutoa takwimu za uchambuzi wa tabianchi. Setilaiti hizo zinafuatilia vyanzo vya maji na uhakika wa chakula.

UNESCO , RFI kupigia chepuo historia ya bara Afrika

Shirika la Elimu ,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na redio ya kimataifa ya Ufaransa RFI, leo wametiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa kihariri wa kupigia chepuo ukusanyaji wa kitabu cha historia ya Afrika.

Taarifa ya UNESCO inasema kuwa katika makubaliano hayo RFI kupitia kipindi chake cha wiki kiitwacho kumbukumbu ya bara kitajikita katika historia ya jumla pamoja na makabiliano dhidi ya chuki inayonyemelea historia ya bara Afrika.

Ban atiwa hofu na mkwamo wa serikali ya mpito Sudan Kusini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-Moon ameelezea hofu yake kuhusu mkwamo kwa pande zote Sudan Kusini dhidi ya kuanzisha majimbo 28 na kushindwa kwao kukamilisha miayadi ya tarehe 22 Januari ya kuanzisha serikali ya mpuito ya Umoja wa kitaifa nchini Sudan Kusini.

Amesisitiza kwamba kuundwa kwa serikali ya mpito ni hatua muhimu katika kutekeleza makubaliano ya Amani na kuweka msingi wa utulivu na Amani ya kudumu nchini humo. Stephane Dijarric ni msemaji wa Umoja wa mataifa

(SAUTI YA DUJARRIC)

WFP yafikisha misaada Yemen

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limefanikiwa kufikisha misaada ya chakula kwenye maeneo yaliyozingirwa mjini Taiz nchini Yemen ambapo watu wanakumbwa na njaa.

Kwa mujibu wa taarifa ya WFP iliyotolewa leo, msafara wa WFP umepeleka vyakula vya mwezi mmoja kwa familia 3,000 baada ya kutimiza mazungumzo na pande kinzani za mzozo kuhusu umuhimu wa kuruhusu misaada ya kibinadamu,

WFP imeongeza kwamba mjini Taiz, maisha ya familia moja kati ya tano yako hatarini kwa sababu ya utapiamlo.

Kwa ujumla, watu milioni 7.6 nchini Yemen wanakumbwa na njaa.

MONUSCO bado kuamua kuhusu usaidizi wake kwa uchaguzi DRC

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC, MONUSCO umeeleza utayari wake wa kusaidia tume ya kitaifa ya uchaguzi CENI katika maandalizi ya uchaguzi nchini humo lakini bado kiwango cha usaidizi chapaswa kuamuliwa.

Hii ni kwa mujibu wa video zilizotolewa na MONUSCO baada ya ziara ya rais wa CENI kwenye eneo la Kivu Kaskazini ili kutathmini hali ya maandalizi ya mchakato wa mapitio ya daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kasi ya kuenea kwa kirusi cha Zika inatutia hofu- WHO

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO Dkt. Margaret Chan amesema taarifa za kuenea kwa kasi kwa kirusi cha Zika zinatia hofu kubwa .

Akizungumza kwenye kikao cha bodi ya wakurugenzi ya WHO, Dkt, Chan amesema hofu hiyo inazingatia uwezekano wa uhusiano unaodaiwa kuwepo kati ya kirusi hicho na watoto wanaozaliwa na vichwa vidogo.

Amesema ingawa hadi sasa hakuna uthitisho wa uhusiano kati ya kirusi hicho na watoto kuzaliwa na vichwa vidogo…

(Sauti ya Dkt, Chan)

Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Lebanon Sigrid Kaag azuru Iran

Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Lebanon Bi. Sigrid Kaag, Jumapili amekutana na maafisa wa serikali ya Iran mjini Tehran.

Mratibu huyo maalumu amejadili na maafisa wa serikali kuhusu hali ya kisiasa nchini Lebanon, maendeleo ya kikanda yanayoathiri Lebanon na juhudi za kuchagiza utulivu na usalama katika kanda nzima.

Wakati za ziara hiyo Bi Kaag pia amekutana na wawakilishi wa jumuiya ya kidiplomasia. Ziara yake nchini Iran imefanyika kama sehemu ya majadiliano yanayoendelea na mratibu huyo maalumu na wadau wengine muhimu katika kanda.

UN Photo - Jean-Marc Ferre

Mazungumzo kuhusu Syria yasogezwa hadi Ijumaa: de Mistura

Mazungumzo kuhusu Syria yaliyokuwa yaanze leo, Geneva, Uswisi, yamesogezwa mbele hadi Ijumaa wiki hii ya tarehe 29.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura ametangaza hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva akisema yatafanyika kwa miezi Sita.

Amesema mialiko kwa washiriki inatarajiwa kuanza kusambazwa Jumanne na kwamba majadiliano kuhusu washiriki wa mazungumzo hayo baina ya wasyria bado yanaendelea.

(Sauti ya de Mistura)

WMO yathibitisha mwaka 2015 umevunja rekodi ya joto duniani:

Shirika la kimataifa la utabiri wa hali ya hewa WMO limethibitisha kwamba wastani wa joto kimatifa kwa mwaka 2015 umevunja rekodi zote zilizopita kwa kiwango cha nyuzi joto 0.76C iki ni juu ya wastani wa mwaka 1961-1990 .

Kwa mujibu wa WMO kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 2015 kiwango cha joto kilikuwa nyuzi joto 1 Selisiasi juu ya kile kilichokuwa kabla ya zama za viwanda.