Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Kiongozi wa OCHA aangazia hali ya kibinadamu Eritrea na Ethiopia

Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, Kyung-wha Kang, amehitimisha ziara ya siku tatu nchini Eritrea akisihi jumuiya ya kimataifa kuongeza usaidizi wake kwa watu wanaoishi kwenye mazingira magumu nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Bi Kang amekutana na viongozi wa serikali na kutembelea vituo vya afya vinavyoongozwa na serikali kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, akishuhudia hatua zilizopigwa na serikali katika kuimarisha afya ya mama na mtoto.

Ban akaribisha muafaka Somalia kuhusu mfumo wa serikali baada ya uchaguzi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha uamuzi uliofanywa leo na serikali kuu ya Somalia kuhusu mfumo wa serikali mpya itakayowekwa na mchakato wa uchaguzi baadaye mwaka huu, ambayo itakuwa jumuishi na shirikishi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Ban amewapa heko viongozi wa Somalia kufuatia uamuzi huo, ambao amesema unafungua njia ya kuhamisha madaraka kwa wakati upasao mwishoni mwa muhula wa serikali ya sasa.

UNECE, UNITAR zaanzisha ubia wa kutekeleza SDGs

Katika kuwezesha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs, taasisi mbili za Umoja wa Mataifa mjini Geneva zimeanzisha ubia ili kukuza viwango na uwezo katika kufikia melengo hayo.

Taasisi hizo ambazo ni kamisheni ya uchumi ya bara Ulaya  UNECE na taasisi ya mafunzo na utafiti UNITAR kwa pamoja katika taarifa zimeeleza kuwa maeneo yatakayopewa kipaumbele  katika jitihada za pamoja ni ubia katika taasisi binafsi za umma, usalama barabarani na mazingira.

OECD na UNHCR watoa wito wa kuongeza sera za kuwajumuisha wakimbizi:

Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) Ulaya na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR),kwa pamoja wametoa wito kwa serikali kuongeza juhudi za kusaidia wakimbizi kujumuishwa katika jamii na kuchangia katika jamii na uchumi barani Ulaya.

Wakizungumza kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa masuala ya ulinzi na ujumuishi wa wakimbizi mjini Paris wamesema mwaka 2015 watu zaidi ya milioni moja wameingia Ulaya kutafuta hifadhi huku wengine milioni 1.5 wakiomba ukimbizi katika mataifa ya OEDC.

Kobler alaani vikali utekaji wa mbunge Libya, ataka aachiliwe mara moja

Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, UNSMIL, Martin Kobler, amelaani vikali utekaji wa mbunge Mohamed al-Ra’id, na kutaka mbunge huyo aachiwe huru mara moja bila masharti yoyote.

Bwana al-Ra’id alitekwa nyara hapo jana akiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege, baada ya kushiriki kikao cha wawakilishi wa bunge huko Tobruk.

Kobler ameeleza kukerwa na kitendo hicho, na kutoa wito kwa wote wenye ushawishi wafanye kila wawezalo ili kuhakikisha mbunge huyo anaachiliwa.

Hali iliyoko Mashiriki ya Kati si endelevu - Ban akariri

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema kwamba Katibu Mkuu Ban Ki-moon ameshikilia msimamo wake na kukariri kauli aliyoitoa kwenye Baraza la Usalama mnamo Jumanne Januari 26, kuhusu Mchakato wa amani Mashariki ya Kati.

Amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari baada ya maoni kadhaa kuibuka kuhusu hotuba ya Katibu Mkuu, wengine wakimlaumu kwa kutetea ugaidi.

Mapigano Jebel Marra, Darfur yawalazimu maelfu kukimbia makwao

Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Sudan, Marta Ruedas, ameeleza kutiwa wasiwasi na athari za mapigano katika eneo la Jebel Marra katika jimbo la Darfur nchini Sudan, ambako takriban watu 19,000 wamekimbilia jimbo la Darfur Kaskazini, huku wengine 15,000 wakikimbilia jimbo la Darfur ya Kati katika kipindi cha wiki mbili zilizopita. Eneo la Jebel Marra linapatikana katika majimbo matatu ya Darfur.

Baraza la usalama halijajitahidi vya kutosha kuhusu Syria- OCHA

Leo Baraza la Usalama limejadili hali ya kibinadamu nchini Syria, mzozo nchini humo ukikaribia kuingia mwaka wa sita na ripoti zikionyesha kwamba hali inazidi kuzorota.

Akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Usalama, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA Stephen O’Brien amesema OCHA inakadiria kuwa watu wapatao milioni 4.5 hawafikiwi na misaada ya kibinadamu kwenye maeneo yaliyokumbwa na mapigano makali, miongoni mwao nusu milioni wakikumbwa na njaa kwenye maeneo yaliyozingirwa.

UN Photo/Ari Gaitanis

Licha ya Ebola, Sierra Leone yapiga hatua kukuza haki za binadamu

Leo hali ya Sierra Leone ikifanyiwa tathmini ya haki za binadamu kwenye kikao cha Baraza la Haki za Binadamu huko Geneva Uswisi, Waziri wa Sheria wa nchi hiyo Joseph Fitzerald Kamara amesema kwamba mlipuko wa Ebola ulisimamisha kwa muda jitihada za serikali katika kukuza maendeleo na haki za binadamu nchini humo.

Ameeleza kwamba rais alilazimika kutangaza hali ya dharura iliyopiga marufuku shughuli za kijamii na maandamano yote.

Maisha ya upweke kwa wakimbizi wa Syria nchini Lebanon

Mwaka wa sita sasa mzozo wa Syria unaendelea bila ya nuru ya kupata suluhu la kisiasa. Raia wa Syria wamekimbia makazi yao na wamesalia wakimbizi wa ndani na wengi wao wamesaka hifadhi nchi jirani na wengine kuvuka bahari na majangwa  hadi Ulaya. Miongoni mwao ni Jawaher ambaye sasa anaishi Lebanon. Raha ya maisha aliyozoea nchini mwake Syria imegeuka shubiri ambayo hata hana uhakika lini tena itakuwa tamu. Je kulikoni? Assumpta Massoi anafafanua kwenye makala hii.