Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha muafaka Somalia kuhusu mfumo wa serikali baada ya uchaguzi

Ban akaribisha muafaka Somalia kuhusu mfumo wa serikali baada ya uchaguzi

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha uamuzi uliofanywa leo na serikali kuu ya Somalia kuhusu mfumo wa serikali mpya itakayowekwa na mchakato wa uchaguzi baadaye mwaka huu, ambayo itakuwa jumuishi na shirikishi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Ban amewapa heko viongozi wa Somalia kufuatia uamuzi huo, ambao amesema unafungua njia ya kuhamisha madaraka kwa wakati upasao mwishoni mwa muhula wa serikali ya sasa.

Amesifu hasa dhamira ya uwakilishi wa wanawake na makundi ya walio wachache, hususan kwamba wanawake watachukua asilimia 30 ya viti katika bunge lijalo, kulingana na Azimio la Mogadishu la Disemba 2015.

Ban amekariri haja ya dharura ya kuweka ratiba ya kisiasa itakayopelekea kufanyika uchaguzi unaowajumuisha Wasomali wote ifikapo mwaka 2020, ili kuendeleza kasi ya kuleta mabadiliko ya demokrasia nchini humo, akiahidi uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa mchakato wa amani Somalia.

Photo Credit
Bendera ya Somala ikipepea wakati wa kuapishwa kwa wabunge mara ya kwanza nchini humo mwaka 2012.(Picha:UM/Stuart Price)