Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa ufupi: Gaza; Ukraine; Rohingya

Mtoto aliyejeruhiwa anatunzwa katika Hospitali ya Nasser iliyoko Khan Younis.
© UNICEF/Abed Zaqout
Mtoto aliyejeruhiwa anatunzwa katika Hospitali ya Nasser iliyoko Khan Younis.

Habari kwa ufupi: Gaza; Ukraine; Rohingya

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limeonya kwamba watu 570,000 wanakabiliwa na janga kubwa la njaa kutokana na kuendelea kwa mapigano makali huko Gaza, wahudumu wa misaada kunyimwa fursa ya kuwafikia wenye uhitaji na kukatwa kwa mawasiliano, sababu ambazo pia zimeathiri uwezo wa shirika hilo  kufikisha na kusambaza msaada kwa usalama kwa maelfu ya watu. Hivyo limetoa wito wa kuongezwa haraka fursa za usambazaji na ufikishaji wa misaada ya kibinadamu. 

Pia limesema kuna wanawake na wasichana karibu milioni 1 waliotawanywa na vita inayoendelea Gaza na 690,000 kati yao wanahitaji huma ya haraka ya maji safi, vyoo, faragha na taulo za kike.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA limeonya juu ya ongezeko la idadi ya vifo na maeneo ya raia yanayozidi kushambuliwa Khan Younis, huku leo mashambulizi ya mabomu yakiripotiwa karibu na hospitali ya Al Amal.

Boti iliyobeba wakimbizi wa Rohingya kuvuka Bahari ya Andaman imetia nanga baharini baada ya wakimbizi hao kuteremka katika ufuo wa Aceh, Indonesia Januari 8, 2023.
© UNHCR/Kenzie Eagan
Boti iliyobeba wakimbizi wa Rohingya kuvuka Bahari ya Andaman imetia nanga baharini baada ya wakimbizi hao kuteremka katika ufuo wa Aceh, Indonesia Januari 8, 2023.

Wakimbizi wa Rohingya

Kwingineko wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kushughulikia ongezeko kubwa la vifo vya wakimbizi wa Rohingya baharini umetolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Kwa mujibu wa shirika hilo wakimbizi wa Rohngya 569 walipoteza maisha au kupotea walipotumia safari hatari za boti katika bahari ya Andaman na Ghuba ya Bengal mwaka 2023, hiyo ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya waliopoteza Maisha tangu mwaka 2014.

Waokoaji wanafanya kazi katika jengo lililoharibiwa na makombora huko Kyiv.
© UNICEF/Aleksey Filippov
Waokoaji wanafanya kazi katika jengo lililoharibiwa na makombora huko Kyiv.

Vita Ukraine

Nahitimisha na Ukraine ambako mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu wa nchi hiyo Denise Brown amelaani vikali wimbi jipya la mashambulizi ya anga ya Urusi dhidi ya miji iliyo na watu wengi nchini Ukraine.

Bwana Brown amesema asubuhi ya leo mashambulizi makubwa katika maeneo ya makazi ya watu “ Yamesababisha uharibifu katika majengo ya raia yaliyopo karibu na ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Kyiv. Nyumba zimeharibiwa na raia waliokuwa wakijaribu kuendelea na maisha yao hivi sasa wamelazwa hospitali, mashambulzi haya dhidi ya raia lazima yakome.