Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu yetu kuhusu vifo vya watoto Gaza inatimia: UNICEF

Chakula kinagawiwa kwa Wapalestina waliokata tamaa.
© UNRWA
Chakula kinagawiwa kwa Wapalestina waliokata tamaa.

Hofu yetu kuhusu vifo vya watoto Gaza inatimia: UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo limeonya kwamba hofu iliyokuwanayo kuhusu vifo vya watoto Gaza hasa kutokana na kuongezeka kwa utapiamlo imewadia.

Kwa mujibu wa tarifa yake iliyotolewa mjini Amman na mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa shirika hilo Adele Khodr “Takriban watoto kumi wameripotiwa kufa kwa sababu ya upungufu wa maji mwilini na utapiamlo katika Hospitali ya Kamal Adwan katika Ukanda wa Kaskazini wa Gaza katika siku za hivi karibuni. Kuna uwezekano kuna watoto zaidi wanaopigania maisha yao mahali fulani katika hospitali moja iliyobaki ya Gaza, na kuna uwezekano watoto wengi zaidi kaskazini hawawezi kupata huduma kabisa. Vifo hivi vya kusikitisha na vya kutisha vinasababishwa na mwanadamu, vinaweza kutabirika na vinaweza kuzuilika kabisa.”

Khodr ameongeza kuwa "Ukosefu mkubwa wa chakula chenye lishe bora, maji salama na huduma za matibabu, matokeo ya moja kwa moja ya vikwazo vya upatikanaji msaada na hatari nyingi zinazokabili operesheni za kibinadamu za Umoja wa Mataifa, vinaathiri watoto na mama, na kuzuia uwezo wao wa kunyonyesha watoto wao, hasa katika Ukanda wa Kaskazini Gaza. Watu wana njaa, wamechoka na wana kiwewe. Wengi wanahaha kulinda Maisha yao.”

Umoja wa Mataifa unasema Gaza inakabiliwa na mgogoro wa chakula
© UNICEF/Abed Zagout
Umoja wa Mataifa unasema Gaza inakabiliwa na mgogoro wa chakula

Tofauti kubwa kati ya Kaskazini na Kusini mwa Gaza

Mkurugenzi huyo amesema "Kutofautiana kwa hali ya Gaza kaskazini na kusini ni ushahidi wa wazi kwamba vikwazo vya misaada kaskazini vinagharimu maisha.”

Ameongeza kuwa uchunguzi wa eneo la Kaskazini mwa Gaza uliofanywa na UNICEF na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP mwezi Januari uligundua kuwa “karibu asilimia 16 au mtoto 1 kati ya watoto 6 wa umri wa chini ya miaka 2 wana utapiamlo.”

Pia uchunguzi kama huo uliofanywa kusini mwa Rafah, ambapo misaada imekuwa ikipatikana zaidi, uligundua kuwa asilimia 5 ya watoto walio chini ya umri wa miaka 2 wana utapiamlo.

Mkurugenzi huyo ameendelea kusema kwamba mashirika ya misaada ya kibinadamu kama UNICEF “lazima yawezeshwe kubadili janga la kibinadamu, kuzuia njaa, na kuokoa maisha ya watoto. Kwa hili tunahitaji vituo vingi vya kutegemewa ambavyo vitatuwezesha kuleta misaada kupitia njia zote zinazowezekana, ikiwa ni pamoja na kaskazini mwa Gaza na hakikisho la usalama na kupita bila vizuizi ili kusambaza misaada, kwa kiwango kikubwa kote Gaza, bila kukataliwa, kucheleweshwa na vikwazo vya ufikishaji.”

Mjini Gaza watoto wakisubiri kupokea chakula wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea
© UNDP PAPP/Abed Zagout
Mjini Gaza watoto wakisubiri kupokea chakula wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea

UNICEF imekuwa ikionya kuhusu vifo

UNICEF imekuwa ikionya tangu mwezi Oktoba mwaka jana kwamba idadi ya vifo huko Gaza itaongezeka kwa kasi ikiwa janga la kibinadamu litaibuka na kuachwa kuzidi kuendelea. 

“Hali imekuwa mbaya zaidi, na kwa sababu hiyo, wiki iliyopita, tulionya kwamba mlipuko wa vifo vya watoto ulikuwa karibu ikiwa changamoto ya lishe inayoongezeka haitatatuliwa. Sasa, vifo vya watoto tulivyohofia vimewasili hapa na vina uwezekano wa kuongezeka kwa kasi endapo vita havitoisha na vikwazo vya misaada ya kibinadamu kutatatuliwa mara moja.”

Khodr amehitimisha tarifa yake akisema "Hisia ya kutokuwa na msaada na kukata tamaa miongoni mwa wazazi na madaktari katika kutambua kwamba misaada ya kuokoa maisha ipo kilomita chache tu kutoka walipo, inawawekwa mahali pasipofikirika, lazima iwe hali isiyoweza kuvumilika. Lakini kibaya zaidi ni vilio vya uchungu vya watoto hao wanaoangamia polepole wakati ulimwengu ukitazama. Maisha ya maelfu zaidi ya watoto na watoto wachanga yanategemea hatua za haraka zinazochukuliwa sasa.”