Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali si hali hospitali tatu zilizoko Gaza Kaskazini, wajawazito wabebwa kwa machela

Mgonjwa akipatiwa huduma katika chumba cha upasuaji kwenye hospitali ya Al-Quds Gaza
© WHO
Mgonjwa akipatiwa huduma katika chumba cha upasuaji kwenye hospitali ya Al-Quds Gaza

Hali si hali hospitali tatu zilizoko Gaza Kaskazini, wajawazito wabebwa kwa machela

Amani na Usalama

Zaidi ya siku 100 za mapigano makali baina ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, Hamas pamoja na vikundi vingine vilivyojihami huko ukanda wa Gaza, Mashariki ya kati yaliyoanza tarehe 7 mwezi Oktoba mwaka huu, yamesababisha sio tu vifo miongoni mwa wapalestina na waisraeli bali pia kudhoofika kwa mifumo ya afya, halikadhalika uhaba wa misaada muhimu ya kiutu kama vile chakula, maji, huduma za kujisafi na malazi. Hali imekuwa ya kusikitisha zaidi kaskazini mwa Gaza ambako wakazi walipatiwa amri ya kuhama na mashambulizi yakaelekezwa humo. 

Licha ya mapigano, yaliyochochewa na shambulizi la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7 na kusababisha vifo na mateka, baadhi ya wahudumu wa afya walijitolea kwa hali na mali kusalia ili pamoja na uhaba wa vifaa na usalama, kusaidia majeruhi na wengine wanaohitaji huduma kama vile wajawazito.  

Ali, mtoto mvulana mwenye umri wa miaka 11, akitembea juu ya vifusi vya nyumba yake iliyoharibiwa katika Mtaa wa Omar Al-Mukhtar katika Jiji la Gaza.
© UNICEF/Omar Al-Qattaa
Ali, mtoto mvulana mwenye umri wa miaka 11, akitembea juu ya vifusi vya nyumba yake iliyoharibiwa katika Mtaa wa Omar Al-Mukhtar katika Jiji la Gaza.

Magofu! Vifusi vya udongo! Na nondo zilizotapakaa ndio taswira ya Gaza Kaskazini na hususan nje ya hospital ya KAMAL AWDAN, wafanyakazi wa shirika la hilal nyekundu la Palestina wakipita hapa na pale kujionea iwapo kuna chochote cha kunusuru. Ni jengo la hospital ya Kamal Awdan lilipopigwa na makombora kutoka Israel. 

Wahudumu wa afya wamejikusanya na wanajitolea  

Ingawa hivyo ndani katika sehemu ambayo haikukumbwa na mashambulizi, huduma za matibabu zinaendelea. 

Haneen Abu Dayyeh, mtaalamu wa kujitolea wa kutoa dawa za nusu kaputi kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji hapa hospitalini anasema “licha ya suala kwamba wahudumu wa afya hawako tena hapa, baadhi wamechukuliwa, wengine wamefurushwa makwao, au wamekimbilia uhamishoni na wengine wamekamatwa, sisi ambao tumefurushwa makwetu na tunaishi hapa hospitalini kwa kusaidiana na baadhi ya watu wenye ujuzi wa tiba, tunatoa msaada wa matibabu kwa wakimbizi, majeruhi kwa kadri ambavyo tunaweza.” 

Madaktari wa upasuaji wa wakimfanyia upasuaji mgonjwa katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza. (Maktaba)
WHO
Madaktari wa upasuaji wa wakimfanyia upasuaji mgonjwa katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza. (Maktaba)

Wanatoa huduma kwa majeruhi wakiwemo wale waliovunjika miguu ambapo hapa mmoja anawekewa vyuma. 

Katika chumba kingine huduma kwa watoto wachanga waliozaliwa hapa inaendelea. Ukosefu wa nishati ya mafuta kwa ajili ya kuendeshea mitambo ikiwemo ya umeme umesababisha adha sio tu kwa madaktari bali pia kwa watoto wanaozaliwa njiti. 

Dkt. Muhammad Hamoud, mtaalamu wa magonjwa ya watoto anafafanua ya kwamba “hapa tuna dalili za awali za tatizo la afya ubongo kwa mtoto njiti anayehitaji hewa ya oksijeni na mirija ya kumlishia saa zote. Na unaona amevalishwa nguo ingawa yuko ndani ya mashine ya kumwongezea joto. Sababu ni kwamba mashine hii haina joto la kutosha kutokana na ukosefu wa umeme, hivyo tunalazimika kuwavalisha nguo.” 

Daktari Hamoud akizungumza,  kando yuko mama mmoja akimwangalia mwanae mchanga anayepata huduma, pamoja na kufuata huduma, hospitali imegeuka makazi yake akisema mtoto wake ana umri wa siku 12. walifurushwa makwao na kuhamia shuleni ambako mazingira si safi na salama kwake yeye na mtoto wake. 

Uhaba wa nishati na athari hasi hospital ya Al-Awda 

Uhaba wa nishati ya mafuta ya umeme imeathiri pia huduma katika hospitali ya Al Awda hapa kaskazini mwa Gaza ambapo katika Idara ya kuhudumia wajawazito hali ni changamoto sio tu kwa madaktari na wagonjwa bali pia kwa wafamilia wanaoleta mjamzito anayehitaji kujufungua kwa upasuaji.  

Asma Kutkut kutoka idara hii anasema “Kuhusu wagonjwa wanaohitaji upasuaji,  kwa kweli vyumba vya operesheni viko chini ghorofani, yaani unashuka ghorofa mbili. Na suala kwamba hakuna umeme, hivyo lifti haifanyi kazi. Wahudumu wa afya na wanafamilia wanalazimika kumbeba mjamzito kwenye ubao na kushuka kwa ngazi hadi kumfikisha mgonjwa kwenye chumba cha upasuaji. Na hii huleta maumivu kwa mjamizito kwani anashushwa kwenye ngazi akiwa amebebwa badala ya kutumia lifti.” 

Mwanamke akipatiwa huduma katika hospitali ya Al Hilo Gaza baada ya kufukiwa na kifusi na kufanyiwa upasuaji wa kujifungua
© UNFPA/Bisan Ouda
Mwanamke akipatiwa huduma katika hospitali ya Al Hilo Gaza baada ya kufukiwa na kifusi na kufanyiwa upasuaji wa kujifungua

Wanalazimika kutumia nusu kaputi yenye maumivu zaidi kwa wajawazito 

Changamoto nyingine ni ukosefu wa vifaa vya tiba ikiwemo dawa ya kawaida ya nusu kaputi kwa mjamzito anayehitaji upasuaji. Kwa kawaida hupatiwa ile inayohitaji oksijeni na umeme ambapo mgonjwa huzinduka baada ya saa 24. Lakini uhaba wa dawa hiyo umelazimu wawadunge sindano ya nusu kaputi mgongoni ambayo huchukua hadi siku tatu kwa mgonwa kurejea hali ya kawaida. 

Na zaidi ya yote hofu ya mashambulizi imesababisha wajawazito nao kuhofia kufika hospitalini na badala yake wanajifungulia nyumbani. Suala hilo likalazimu hospitali kubonga bongo na kuamua kuwafuata wajawazito majumbani. 

“Tuna vitanda kwa ajili ya wajawazito 20 kwani kwa wastani kwa siku idadi ya wajawazito hapa ni takribani 20. Hata hivyo tatizo la ukosefu wa usafiri limefanya hali kuwa mbayá na wajawazito wakashindwa kufika hospitalini kujifungua” amesema Asma akiongeza kuwa, “imekuwa ni vigumu kwa magari ya wagonjwa kufanya kazi, hivyo wajawazito wakawa wanakuja kwa miguu na wengine kujifungulia nyumbani au barabarani. Kwa hiyo tulilazimika kupeleka nyumbani huduma hii ya kufungua ili kuhakikisha wanajifungua salama.” 

Wagonjwa wanaohitaji huduma ya kusafishwa figo nao wameathiriwa vibaya na uhaba wa nishati ya mafuta na umeme katika hospitali ya Al-Shifa kaskazini mwa Gaza.  

Ushuhuda unatoka  kwa Amnah Kahlou ambaye hutegemea huduma hizo katika hospitali hii akisema, “nimenusurika kifo takribani mara 10. Nilijaribu kwenda kusini kupata huduma ya kusafisha figo, lakini sikuweza kufika. Kwa hiyo ilibidi nirudi. Ilinichukua muda mrefu kwa hospitali hii ya Al-shifa kufungua tena huduma ya kusafisha figo. Lakini ilipofunguliwa, ilikuwa imefurika wakimbizi, na hivyo ilikuwa vigumu kufika hapa kuhudumiwa. Kupata huduma ya kusafisha figo ni vigumu sana.” 

Daktari Ghazi Al-Yalji wa hapa hospitali ya Al-Shifa anasema huduma imerejea licha ya vikwazo kama vile ukosefu wa mtambo wa kuondoa chumvi kwenye maji yanayohitajika kwenye mashine ya usafishaji wa figo. 

Vikwazo ni pamoja na kukosa mtambo wa kuondoa “chumvi kwenye maji na hatimaye yatumike kwenye mashine za kusafisha figo. Hivyo tunalazimika kununua maji safi na maji ya kunywa. Bila shaka ni gharama ya ziada, lakini tumesisitiza kurejesha huduma kwa kusaka jawabu mbadala, ambalo ni kununua mitambo ya kuondoa chumvi kwenye maji hadi pale mtambo husika utakavyotengenezwa.” 

Watu waliojeruhiwa katika mashambulizi ya mabomu wakisubiri kutibiwa katika hospitali ya Al Shifa, katika mji wa Gaza.
© WHO
Watu waliojeruhiwa katika mashambulizi ya mabomu wakisubiri kutibiwa katika hospitali ya Al Shifa, katika mji wa Gaza.

Angalau nuru imerejea hapa Al-Shifa wiki hii baada ya kuletwa kwa nishati ya mafuta. Dkt. Ahmed Dahir, Mkuu wa ofisi ndogo ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO huko Gaza anaeleza kwamba “mfumo wa afya unahitaji lita 11,500 za nishati ya mafuta. Kiwango hiki kilicholetwa kitatumia angalau kwa siku mbili na hivyo tunahitaji kiwango kikubwa ili tuweze kuendesha huduma zetu za afya kaskazini mwa Gaza na mji mzima wa Gaza.” 

Lakini kama mapigano yataendelea, hali itazidi kuwa mbayá na wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres unasalia ule ule wa sitisho la mapigano kwa misingi ya kiutu na zaidi ya yote anasema “Haki ya wapalestina ya kujenga taifa lao wenyewe huru lazima itambuliwe na wote. Na kitendo cha upande wowote kupinga suluhu ya uwepo wa mataifa mawili lazima ukataliwe.”