Watu saba wamethibitishwa kuwa na Ebola na mmoja kufariki dunia Uganda:WHO
Watu saba wamethibitishwa kuwa na Ebola na mmoja kufariki dunia Uganda:WHO
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO limesema linaongeza juhudi zake za kudhibiti kusambaa kwa mlipuko mpya wa Ebola nchini Uganda ambako hadi sasa wagonjwa saba wa Ebola aina ya sudan wamethibitishwa kikiwemo kifo cha mtu mmoja.
Tangazo hilo limekuja siku mbili baada ya WHO kuthibitisha kisa cha kwanza baada ya shuku ya vifo sita kwenye wilaya ya Mubende mapema mwezi huu.
Watu 43 waliowasiliana kwa karibu wa marehemu hao wameshabainishwa na 10 wanaaminika kuambukizwa virusi hivyo vya Ebola na hivi sasa wanapatiwa matibabu kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa iliyopo Mubende na kufanya hii kuwa mara ya kwanza Uganda kubaini virusi vya Ebola aina ya Sudan tangu mwaka 2012.
Mubende ipo katika mkoa wa Kati nchini Uganda karibu saa mbili kwa usafiri wa gari kutoka mji mkuu Kampala katika barabara yenye pilika nyingi ya kuelekea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Katika eneo hilo kuna mgodi wa dhahabu ambao unavutia watu kutoka sehemu mbalimbali za Uganda pamoja nan chi nyingine.
WHO imeeleza kwamba sababu ya mwenendo wa watu kusafiri sana katika eneo kuna hatari kubwa ya virusi kusambaa zaidi.
Hatua zinazochukuliwa na WHO
Hatua zinazochukuliwa na shirika la WHO dhidi ya mlipuko huo zinahusisha kusambaza vifaa vya matibabu, kutoa vifaa na kupeleka wafanyikazi kusaidia mamlaka ya Uganda katika kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.
Timu ya kiufundi imetumwa katika wilaya ya Mubende kusaidia ufuatiliaji, kuzuia na kudhibiti maambukizi, na pia usimamizi wa wagonjwa waliothibitishwa. Ufuatiliaji unafanywa kwa kasi katika wilaya jirani, na wahudumu wa ndani wa afya wako mstari wa mbele, ili kuimarisha juhudi za kupambana na Ebola. Wataalam watano wa kimataifa pia wanatumwa, na wengine zaidi wako tayari Kwenda ikiwa wanahitajika.
"Tunachukua hatua za haraka na madhubuti kuhakikisha udhibiti wa mlipuko huu. Utayari wa dharura wa nyumbani wa Afrika unaonekana kuwa muhimu zaidi katika kukabiliana na milipuko kama vile Ebola" amesema Dkt. Abdou Salam Gueye, mkurugenzi wa dharura wa kanda katika ofisi ya WHO Kanda ya Afrika.
Maendeleo ya chanjo
WHO imesema Ebola inaweza kuwa mbaya, lakini utambuzi wa mapema wa dalili na wagonjwa huongeza sana fursa za watu kuishi.
Hakuna chanjo yoyote miongoni mwa chanjo zilizopo sasa za Ebola yenye ufanisi dhidi ya aina ya Sudan iliyotgundulika nchini Uganda, lakini angalau kuna chanjo sita ambazo ziko katika hatua tofauti za maendeleo ya kutengenezwa.
Timu ya mpango wa utafiti na maendeleo ya WHO inawasiliana na watengenezaji wote wa chanjo na inaongoza juhudi shirikishi zinayohusisha wataalam wa kimataifa ili kubaini ni chanjo gani inaweza kufaa kwa tathmini ya ziada wakati wa mlipuko huu, ikiwa wagonjwa zaidi watathibitishwa.