Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya watu 1000 kunusurika na Ebola DRC mapambano vita dhidi ya ugonjwa huo vinaendelea:WHO/WFP/UNICEF

Manusura wa Ebola akifanya kazi katika kituo cha kulea watoto katika eneo la Butembo mashariki mwa DRC (Agosti 2019)
UN Photo/Martine Perret
Manusura wa Ebola akifanya kazi katika kituo cha kulea watoto katika eneo la Butembo mashariki mwa DRC (Agosti 2019)

Licha ya watu 1000 kunusurika na Ebola DRC mapambano vita dhidi ya ugonjwa huo vinaendelea:WHO/WFP/UNICEF

Afya

Wakati manusura wa 1000 wa ugonjwa Ebola ameruhusiwa kwenda nyumbani leo mashirika ya Umoja wa Mataifa yanafanya kila liwezekanalo kuzuia mlipuko unaoendelea wa ugonjwa huo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 

Mashirika hayo hayo lile la afya duniani WHO, la mpango wa chakula duniani WFP, la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la kimataifa Save the children leo wamepongeza uongozi bora wa wizara ya afya ya DRC maelfu ya wahudumu wa afya na washirika wao kwa pamoja wanafanya kazi bila kuchoka na sasa wamesaidia kuokoa maisha ya watu 1000 kutokana na ugonjwa huo hatari wa Ebola.

Mmoja wa manusara hao aliyekabidhiwa cheti cha kunusurika Ebola na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mwezi Septemba ni Kavira ambaye anasema “sikufikiria ningenusurika lakini sasa nimepona, ninataka kurudi katika jamii yangu na kuwaanbia wenzangu watafute matibabu ikiwa wataambukizwa kwa kuwa unaweza kupona.

Kwa mujibu wa Dkt. Ibrahim Soce Fall mkurugenzi msaidizi wa masuala ya dharura wa WHO, ingawa huu ndio mlipuko ulioenda kwa muda mrefu zaidi DRC kuna nyenzo mpya sasa kuweza kuzuia ugonjwa huo “Tuna nyenzo, chanjo n atiba lakini pia bado  tunahitaji kusaka na kumsaidia kila mtu ambaye amekutana na mgonjwa wa Ebola ili kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi zaidi.”

Mlipuko huo uliotangazwa Agosti mosi 2018, ulianzia Kivu Kaskazini na tangu wakati huo umesambaa kwenda maeneo ya Ituri huku kesi zikitangazwa katika mkoa wa Kivu Kusini.

Kupitia mpango ulioongozwa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Mataifa ulifanya jitihada mwezi Mei kuunga mkono serikali ya DRC katika sekta za afya ya umma, kwa kusaidia jamiia zilizoathiriwa na Ebola, katika usalama, masuala ya siasa na usimamizi ya fedha.

Kila manusura hutupa sababu na motisha ya kuendelea kupambana na maradhi ya Ebola, lakini pia manusura ni kumbusho kuwa kuna maisha ambayo hatuwezi kuokoa, alisema David Gressly mratibu wa huduma za dharura dhidi ya ugonjwa wa Ebola.

 Ameongeza kuwa kukukubali kwa watu katika miji kama Rwangoma au Mabolio imechangia kupungua sana visa vya Ebola maeneo hayo.

 Wakiongozwa na UNICEF na kuungwa na mkono na washirika wa kimataifa, maelfu ya wacongo wa kujitolea na washirika kutoka jamii zilizoathirika, wanashirikiana na viongozi wa dini, vyombo vya habari na manusura wa Ebola kueneza habari muhimu kuhusu dalili, kuzuia na matibabu kwa jamii zilizo kwenye hatari ya juu.

Watoto ni kati ya wale walioathirika zaidi  katika jamii, kwa kuwa sio tu wako katika hatari wa kuambukizwa virusi bali pia wao huathiriwa ikiwa wanapoteza wazazi wao au shule kufungwa.

Shirika la Save the Children na mashirika mengine yanawafikia watoto kuwaelimisha kuhusu jinsi za kuzuia kuambukizwa Ebola kupitia hamasisho shuleni na makundi ya vijana.

Licha ya kuwa mkurupuko huu ndio umekuwa kwa muda mrefu zaidi nchini DRC, vifaa vipya sasa vipo kusaidia kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo na kuokoa maisha.  Chanjo hiyo bora zaidi kwa 97.5 imewakinga zaidi ya watu 220,000.