Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia lazima iendelee kufadhili vita dhidi ya Ebola:WHO

Wafanyakazi wa kituo cha Ebola cha Katwa Butembo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakisafisha viatu na nguo
UN Photo/Martine Perret
Wafanyakazi wa kituo cha Ebola cha Katwa Butembo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakisafisha viatu na nguo

Dunia lazima iendelee kufadhili vita dhidi ya Ebola:WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema dunia ni lazima iendelee kufadhili vita dhidi ya Ebola na lisifanyike kosa lolote la kubweteka kwani madhara yake yatakuwa makubwa. 

Wito huo umetolewa na mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus akizungumza na waandishi wa wa habari mjini Geneva Uswis kuhusu hali ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Dkt. Tedros amesema “ingawa dunia hivi sasa imejikita zaidi na virusi vya Corona lakini hatuwezi na hatupaswi kusahau kuhusu Ebola.”

DRC inakabiliwa na mlipuko wa Ebola ambao ni wa pili kwa ukubwa duniani katika historia na ambao yatari umeshakatili maisha ya watu 2200 na visa 3300 kuthibitishwa tangu ulipozuka na kutangazwa rasmi August Mosi 2018.

Hata hivyo mkuu huyo wa WHO amesema “Tunatiwa moyo na mwenendo wa sasa , kumekuwa na visa vitatu tuu kwa wiki nzima iliyopita na hakujakuwa na kisa chochote katika siku tatu zilizopita.”

Pia Dkt. Tedros ameonya kwamba “Hadi pale ambapo hatutakuwa na kisa chochote kwa siku 42 , ugonjwa huu haujakwisha, kama mnavyojua kisa kimoja tu kinaweza kuwasha moto wa mlipuko mwingine na hali ya usalalama Mashariki mwa DRC bado ni tete, hivyo tunayachukulia maendeleo haya mapya kwa tahadhari kubwa ingawa ni mafanikio makubwa.”

Amesisitiza kwamba “dunia ni lazima iendelee kufadhili juhudi za kupambana na Ebola kwani kuodoa mguu tu katika vita hivyo sasa litakuwa kubwa la jinai lenye athari mbayá” Kiwango cha wastani cha vifo vya Ebola ni karibu alimia 50%. Walakini, viwango vya vifo vimetofautiana kutoka 25% hadi 90% katika milipuko iliyopita.

Ebola ilibainika kwa mara ya kwanza mwaka 1976 na kumekuwa na visa na vifo vingi katika mlipuko wa sasa kuliko milipuko yote iliyopita kwa ujumla.